Subscribe Us

Breaking News

Hamas yawaachia huru mateka sita wa Israel

Kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas limewaachia huru Jumamosi mateka sita wa Israel na kuwakabidhi kwa maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu huku Israel ikitarajiwa kuwaachia mamia ya wafungwa wa Kipalestina.

Mateka sita wa Israel walioachiwa huru Jumamosi (22.02.2025) na kundi la Hamas
Mateka Mapema siku ya Jumamosi, Hamas iliwaachia huru kutoka Rafah mateka wawili wa Israel waliofahamika kama Tal Shoham na Averu Mengistuna. Mateka wengine wanne, Omer Shem-Tov, Eliya Cohen, Omer Wenkert, na Hisham al-Sayed, waliachiliwa baadaye huko Nuseirat katikati mwa Gaza.

Mateka wa sita aliyeachiwa mwishoni alifahamikwa kwa jina la Hisham al-Sayed (37) pia baadaye alikabidhiwa kwa Shirika la Msalaba Mwekundu. Hisham alikuwa akishikiliwa mateka na Hamas kwa zaidi ya miaka 10. Israel itatakiwa pia kuwaachilia mamia ya wafungwa wa Kipalestina wanaokadiriwa kufikia idadi ya 600.

Soma pia: Makabidhiano ya miili ya mateka wa Israel yakosolewa

Mabadilishano hayo ya mateka na wafungwa ni sehemu ya makubaliano ya usitishwaji mapigano huko Gaza. Hamas imesema Jumamosi kuwa iko tayari kutekeleza awamu ya pili ya mpango wa makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza, awamu ambayo itatakiwa kuendeleza hatua za kubadilishana mateka na wafungwa na kusitisha kabisa vita huko Gaza huku vikosi vya Israel vikijiondoa kabisa katika Ukanda huo.

Israel: Mwili wa mateka uliokabidhiwa ni wa Shiri Bibas

Israel imethibitisha siku ya Jumamosi kuwa mwili uliokabidhiwa jana na kundi la Hamas ni wa mateka mwanamke Shiri Bibas na hivyo kumaliza hali ya mkanganyiko.

Picha za mateka wa Israel waliofariki Shiri Bibas na wanawe
Pic A

Siku ya Ijumaa, Waziri Mkuu wa IsraelBenjamin Netanyahu  aliilaumu Hamas kwa kushindwa kukabidhi mwili wa mwanamke huyo  aliyetekwa nyara na kundi hilo na kuahidi kuchukua hatua kali.

Siku ya Ijumaa, huzuni ilitawala huko Israel baada ya jeshi kutangaza kuwa mmoja wa miili iliyorejeshwa na Hamas siku ya Alhamisi haukuwa wa bi Shiri Bibas, mama wa watoto wawili wadogo waliokuwa wakihofiwa kufariki kwa muda mrefu.

"Jumamosi asubuhi tulipokea habari tulizoziogopa zaidi. Shiri wetu aliuawa akiwa kifungoni na sasa amerejea nyumbani kwa wanawe, mume, dada yake na familia yake yote kupumzika. Licha ya hofu yetu juu ya hatima yao, tuliendelea kutumaini kwamba tungewakumbatia, lakini sasa tuna uchungu na huzuni," alisema mwanafamilia.

Familia ya Bibas, akiwemo mume wake Yarden Bibas, na watoto wao Ariel (4) na Kfir (miezi 9), wamekuwa ishara yenye nguvu inayodhihirisha majonzi makubwa ya kitaifa kufuatia shambulio baya la Hamas dhidi ya Israel Oktoba 7, 2023.


ليست هناك تعليقات