Kampuni ya dawa ya India inavyochochea matumizi ya dawa za kulevya Afrika Magharibi
Uchunguzi wa BBC Eye umebaini kuwa kampuni ya dawa kutoka India inatengeneza dawa zisizo na leseni, zinazolevya na kuzisafirisha kinyume cha sheria hadi Afrika Magharibi ambako zinasababisha tatizo mkubwa kwa afya ya umma katika nchi zikiwemo Ghana, Nigeria na Cote D'Ivoire.
Kampuni ya Aveo Pharmaceuticals, iliyoko Mumbai, hutengeneza aina mbalimbali za vidonge ambavyo huvipa majina na chapa tofauti na kuviweka kwenye paketi ili kuonekana kama dawa halali. Lakini dawa zote hizo ni mchanganyiko huo huo wa tapentadol (dawa inayolevya) na carisoprodol (dawa ya kutuliza misuli ambayo ina uraibu na imepigwa marufuku Ulaya.)
Mchanganyiko huu wa dawa haujaidhinishwa kutumiwa popote duniani na unaweza kusababisha matatizo ya kupumua na kifafa. Ukiitumia sana inaweza kukuua. Licha ya hatari hizo, dawa hizi za kulevya ni maarufu mitaani katika nchi nyingi za Afrika Magharibi, kwa sababu ni nafuu sana na zinapatikana kwa wingi.
BBC ilipata pakiti zake, zikiwa na nembo ya Aveo, zinazouzwa katika mitaa ya miji ya Ghana, Nigeria, na Ivory Coast.
Baada ya kufuatilia dawa hizo katika kiwanda cha Aveo nchini India, BBC ilituma shushushu ndani ya kiwanda hicho, akijifanya kama mfanyabiashara Mwafrika anayetaka kusambaza dawa za kulevya nchini Nigeria. Kwa kutumia kamera iliyofichwa, BBC ilimrekodi mmoja wa wakurugenzi wa Aveo, Vinod Sharma, akionyesha dawa hiyo hatari ambayo BBC ilikuta ikiuzwa kote Afrika Magharibi.
Katika video iliyorekodiwa kwa siri, shushushu huyo anamwambia Sharma kwamba mpango wake ni kuuza tembe hizo kwa vijana nchini Nigeria "ambao wote wanapenda bidhaa hii."
Sharma hakusita, akajibu. "Sawa," kabla ya kueleza kwamba ikiwa watumiaji watachukua vidonge viwili au vitatu kwa wakati mmoja, wanaweza "kupumzika" na anakubali wanaweza "kulewa." Kufikia mwisho wa mkutano huo, Sharma anasema: "Hii ni hatari sana kwa afya," na kuongeza "siku hizi, hii ni biashara."
ليست هناك تعليقات