Subscribe Us

Breaking News

JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI YAZINDUA KITUO CHA TIBA YA USAFIRI WA ANGA (CAM), KUBORESHA USALAMA WA ANGA KIKANDA



Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Uangalizi wa Usalama wa Usafiri wa Anga wa Afrika Mashariki (CASSOA), Salim Msangi, amehudhuria uzinduzi wa Kituo cha Tiba ya Usafiri wa Anga (CAM). Uwepo wa Bw.Msangi katika hafla hiyo unaonyesha dhamira ya Tanzania katika kuimarisha usimamizi wa tiba katika usafiri wa anga na usalama wa anga katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Bw.Msangi amesisitiza juu ya umuhimu wa CAM katika kuziba mapengo yaliyopo kwenye maeneo ya tiba ya usafiri wa anga na utendaji wa binadamu katika sekta ya usafiri wa anga. Alibainisha kuwa kituo hicho kitaboresha tathmini za tiba ya usafiri wa anga, usimamizi wa usalama, na uchunguzi wa ajali, kuhakikisha kuwa viwango vya kimataifa vya tiba ya usafiri wa anga vinazingatiwa.

Hafla hiyo, iliyofanyika katika Makao Makuu ya CAM katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), iliongozwa na Katibu wa Mkuu kutoka Idara ya Usafirishaji nchini Kenya, Bw. Mohamed Daghar. Tukio hilo liliwakutanisha viongozi mbalimbali wa sekta ya anga, mamlaka za udhibiti, na wadau wa sekta hiyo kutoka kanda nzima.

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Kenya (KCAA) na CASSOA, ilianzisha CAM kama kituo cha kwanza cha tiba ya usafiri wa anga cha kikanda barani Afrika. Tofauti na vituo vya tiba ya usafiri wa anga vya kitaifa vinavyosimamiwa na Mamlaka za Udhibiti wa Usafiri wa Anga za kila nchi, CAM inafanya kazi kama taasisi ya kikanda inayojitegemea, ikitoa usimamizi wa tiba ya usafiri wa anga ulio sanifu kwa Nchi nane wanachama wa EAC.

CAM itatoa mafunzo, utafiti, na msaada wa sera kwa nchi anachama wa EAC, kuhakikisha kuwa taratibu za tiba ya anga zinaendana na viwango vya kimataifa. Pia itaongoza marekebisho ya kanuni na maandiko ya kiufundi ili kuboresha usimamizi wa tiba ya usafiri wa anga katika ukanda wa EAC.

Sambamba na hilo, CAM pia itasaidia katika uchunguzi wa ajali za ndege, ikiwa ni pamoja na uchambuzi wa sumu, ili kubaini uwezekano wa matatizo ya kiafya au matumizi ya vitu vyenye madhara. Pia kitafanya kazi kama kituo cha ushauri kwa kesi ngumu za tiba yausafiri wa anga ambazo zinahitaji utaalamu wa ziada kuliko uwezo wa kila nchi mwanachama.

Kituo hiki kitafanya uchunguzi wa kisayansi wa hali ya juu wa tiba ya usafiri wa anga, ambao huenda usipatikane katika baadhi ya nchi za EAC, kwa kutumia wataalamu wa tiba ya usafiri wa anga wa kikanda. Aidha, CAM itashirikiana na taasisi za kimataifa za tiba ya usafiri wa anga ili kuendeleza utafiti na mbinu bora za matibabu katika sekta ya usafiri wa anga.

Kuanzishwa kwa CAM kumefuatia mapendekezo ya ukaguzi wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), ambalo lilibainisha upungufu katika usimamizi wa tiba ya usafiri wa anga katika nchi wanachama wa EAC. Kituo hicho kinalenga kushughulikia changamoto hizo kwa kuhakikisha kuwa wahudumu wa sekta ya anga wanapata msaada bora wa tiba ya usafiri wa anga.

Kupitia juhudi hizi, EAC inaendelea kuimarisha usalama wa anga, kuhakikisha utoaji wa huduma sanifu za tiba ya usafiri wa anga katika ukanda mzima.
02

01

03

4

No comments