Mzozo wa DRC: Waasi waziacha hoi familia za Wacongo, vita vikipamba moto

Heshima anajikunja kwa maumivu anapojaribu kubadilisha upande wa kulala, jasho linamtoka. Ni mtoto mwenye umri wa miaka 13, amelala kwenye kitanda kwenye hema katika uwanja wa hospitali uliojaa watu katika mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Mguu wa kushoto wa Heshima umefungwa bendeji, tumbo lake lina alama za kuungua, na wazazi wake wote wawili wameuawa.
Jamaa yake, aitwaye Tantine, anatuambia ni nani wa kulaumiwa; waasi wa M23 - wakiungwa mkono na Rwanda ambao wanapambana na jeshi la Congo, linalojulikana kama FARDC. Waasi hao sasa wanadhibiti miji miwili mikubwa katika eneo hili lenye utajiri mkubwa wa madini, ambalo linapakana na Rwanda.
"Ilikuwa Jumapili," anasema. "Kulikuwa na mapigano kati ya waasi na FARDC. (Waasi) walirusha bomu, na nikapoteza watu sita wa familia yangu."


No comments