China yasema iko tayari kwa vita ya aina yoyote na Marekani

China yaionya Marekani kwamba iko tayari kupigana vita ya "aina yoyote" baada ya kujibu vikwazo vya kibiashara vilivyotangazwa na Donald Trump
China imeionya Marekani kuwa iko tayari kupigana "aina yoyote" ya vita baada ya kujibu vikali vikwazo vya biashara vinavyoongezeka vya Rais Donald Trump.
Nchi mbili zenye uchumi mkubwa zaidi duniani zimekaribia kuingia kwenye vita vya kibiashara baada ya Trump kuweka vikwazo zaidi vya kibiashara kwa bidhaa zote za China. China ilijibu haraka kwa kuweka vikwazo (ushuru) wa asilimia 10-15 kwa bidhaa za kilimo za Marekani.
Ubalozi wa China mjini Washington, katika chapisho lake kwenye mtandao wa X, ulisema: "Ikiwa vita ndivyo Marekani inavyotaka, iwe ni vita vya ushuru, vita vya biashara au aina nyingine yoyote ya vita, tuko tayari kupigana hadi mwisho."
Hii ni moja ya kauli kali zaidi kutoka China tangu Trump alipoingia madarakani na inakuja wakati viongozi wakuu wamekusanyika huko Beijing kwa ufunguzi wa Bunge la kitaifa la watu la kila mwaka. Jumatano, Waziri Mkuu wa China Li Qiang alitangaza kuwa China itaongeza tena bajeti yake ya ulinzi kwa asilimia 7.2 mwaka huu na akaonya kuwa "mabadiliko ambayo hayajaonekana katika karne moja yanatokea duniani kwa kasi zaidi." Ongezeko hili lilitarajiwa na linafanana na takwimu iliyotangazwa mwaka jana.
Viongozi mjini Beijing wanajaribu kuwatumia ujumbe watu nchini China kwamba
China imekuwa ikisisitiza kuonyesha picha ya kuwa nchi yenye utulivu na amani tofauti na Marekani, ambayo Beijing inaituhumu kuhusika katika vita Mashariki ya kati na Ukraine.
China pia inaweza kuwa na matumaini ya kunufaika na hatua za Trump zinazohusu washirika wa Marekani kama vile Canada na Mexico, ambazo pia zimeathiriwa na vikwazo vya biashara, na haitataka kuongeza sana kauli kali ili kuwatisha washirika wapya wa kimataifa.
Hotuba ya Waziri Mkuu mjini Beijing siku ya Jumanne ilisisitiza kuwa China itaendelea kufunguka na ina matumaini ya kuvutia uwekezaji zaidi wa kigeni.
China, hapo awali, imesisitiza kuwa iko tayari kwenda vitani. Oktoba mwaka jana, Rais Xi alitoa wito kwa wanajeshi kuimarisha utayari wao wa vita walipokuwa wakifanya mazoezi ya kijeshi karibu na kisiwa kinachojitawala cha Taiwan. Lakini kuna tofauti kati ya utayari wa kijeshi na utayari wa kwenda vitani.

Chapisho la ubalozi wa China mjini Washington lilinukuu taarifa ya wizara ya mambo ya nje kwa Kiingereza kutoka siku iliyotangulia, ambayo pia ilituhumu Marekani kuilaumu China kwa kuingizwa kwa dawa ya fentanyl.
"Suala la fentanyl ni kisingizio dhaifu cha kuongeza vikwazo vya Marekani kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka China," msemaji wa wizara ya mambo ya nje alisema.
"Vitisho havitutishi. Uonevu haufanyi kazi kwetu. Shinikizo, kulazimisha au vitisho sio njia sahihi ya kushughulika na China," aliongeza.
Uhusiano wa Marekani na China daima ni mojawapo ya migogoro mikubwa zaidi duniani. Chapisho hili kwenye X limesambazwa sana na linaweza kutumiwa na "China hawks" (wachochezi dhidi ya China) katika baraza la mawaziri la Trump kama ushahidi kwamba Beijing ni tishio kubwa zaidi la sera ya kigeni na kiuchumi kwa Washington.
Maafisa mjini Beijing walikuwa na matumaini kwamba uhusiano wa Marekani na China chini ya Trump unaweza kuanza kwa urafiki zaidi baada ya kumwalika Xi kwenye kuapishwa kwake. Trump pia alisema viongozi hao wawili walikuwa na "mazungumzo mazuri ya simu" siku chache tu kabla ya kuingia Ikulu.
Kulikuwa na ripoti kwamba viongozi hao wawili walikuwa wafanye mazungumzo mengine ya simu mwezi uliopita. Hilo haikutokea.
Xi tayari alikuwa akipambana na matumizi duni yanayoendelea, mgogoro wa mali na ukosefu wa ajira.
China imeapa kuwekeza mabilioni ya dola katika uchumi wake unaodorora na viongozi wake walitambulisha mpango huo huku maelfu ya wajumbe wakihudhuria Bunge la kitaifa la watu, bunge la kupitisha maamuzi yaliyokwisha fanywa nyuma ya pazia.
China ina bajeti ya pili kwa ukubwa ya kijeshi duniani kwa dola bilioni 245 lakini ni ndogo sana kuliko ile ya Marekani. Beijing hutumia asilimia 1.6 ya Pato la Taifa kwa jeshi lake, chini sana kuliko Marekani au Urusi, kulingana na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm.
Hata hivyo, wachambuzi wanaamini China inapunguza kiasi inachotumia kwenye ulinzi.


No comments