SIMBA imeendelea kuipa ugumu kazi yake ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kushindwa kuvuna alama tatu dhidi ya Azam FC, kufuatia kutoka sare ya bila kufungana katika mchezo huo.
Katika pambano hilo, Azam FC walikuwa nyumbani wakiikaribisha Simba, huku kila timu ikilazimika kuridhika na alama moja. Matokeo hayo yamewaacha wenyeji wakiendelea kushika nafasi ya tatu wakiwa na alama 33 kwenye msimamo wa ligi.
Kwa upande wa Simba, sare hiyo imeifanya ibaki katika nafasi ya pili ikiwa na alama 35 baada ya kucheza michezo 16, huku vinara Yanga wakiwa mbele kwa alama 41 wakicheza michezo 17.
Hali hiyo inaifanya Simba kubaki nyuma kwa tofauti ya alama sita, licha ya kuwa na mchezo mmoja wa kiporo dhidi ya Tabora United.
Matokeo hayo yanaipa Yanga nafasi nzuri zaidi ya kujipanga na kujiimarisha katika mbio za kutetea ubingwa wao wa ligi, huku presha ikizidi kuongezeka kwa upande wa Simba katika harakati za kuwasaka vinara hao.
Katika mchezo huo, kipindi cha kwanza kilimalizika bila timu yoyote kufanikiwa kutikisa nyavu. Azam FC walionekana kuwa imara zaidi katika safu ya ulinzi licha ya kujaribu kushambulia mara kadhaa.
0 Comments