Gallery

2/04/2025

 g

CHANZO CHA PICHA,AFP

Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda sasa wanaudhibiti na kuuendesha mji wa Goma ambao ndio mkubwa na muhimu zaidi katika eneo la mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).

Mji wa Goma ndio makao makuu ya kiutawala wa jimbo la Kivu Kaskazini na baada ya Kinshasa na Lubumbashi, Goma ni mji wa tatu kwa ukubwa nchini DRC. Pia ni kitovu cha biashara kubwa ya madini ikiwa ni pamoja na dhahabu, coltan, bati na biashara za madini mengine kutoka migodi tajiri huko Masisi, Walikale na kwingineko katika mkoa huo.

Ni makao ya mashirika mengi ya kimataifa ya misaada na ni kituo cha jeshi la Umoja wa Mataifa jeshi kubwa zaidi la Umoja wa Mataifa la kulinda amani (MONUSCO) Pamoja na vikosi vya Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Africa (SADC) kutoka Afrika Kusini, Tanzania, na Malawi vipo katika mji huo.

Hivyo, kuanguka kwa Goma ni dhahiri kuwa ni pigo kubwa kwa serikali ya Kinshasa pamoja na washirika wake. Lakini pia hatua muhimu ya kusukuma ajenda ya kundi la M23 pamoja na washirika wake katika mgogoro wao na serikali ya nchi hiyo.

Swali muhimu zaidi ni kuwa wakati vita ikiendelea – japo M23 wametangaza kusitisha mapigano wakati wakiwa njiani kujaribu kuuteka mji mwingine muhimu wa Bukavu uliopo katika jimbo la Kivu Kusini – je, M23 kuiteka Goma pamoja na miji na vijiji vingine katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini kunaweza kuleta suluhu ya vita?

Je, kutekwa kwa mji wa Goma mara hii kutaleta mabadiliko yoyote?

g

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Kujibu swali hili ni muhimu kuangalia kiini cha mzozo wenyewe kwani hii ni mara ya pili kwa M23 kuuteka mji wa Goma. Mnamo mwezi wa Novemba, 2012, M23 iliuteka mji huu kwa siku 10, baada ya majeshi ya DRC kuutoroka, lakini baadaye waliondoshwa na kikosi maalumu cha kulinda amani cha kikanda kilichokuwa chini ya mwamvuli wa MONUSCO ambacho kilijumuisha wanajeshi wa Tanzania, Afrika Kusini na Malawi.

Hali inavyoonesha ni kuwa mwaka huu – tofauti na ilivyokuwa mwaka 2012 – M23 hawana mpango wa kuishikilia Goma kwa muda mfupi –kwa kuwa tayari wamesogeza mstari wa mbele wa mapambano kuelekea Bukavu. Japo katika tangazo lao la kusitisha mapigano la Jumatatu usiku wametangaza kuwa hawana nia ya kuuteka mji wa Bukavu.

Lakini katika tangazo hilo hilo, wamelaani kile walichodai ni jeshi la Kongo kutuma ndege za kivita "kuua watu katika maeneo ambayo yamekombolewa." Kwa mujibu wa M23, ndege hizo zinatokea katika kiwanja cha ndege cha Kavumu ambacho kipo karibu na Bukavu.

M23 pia wameendelea kusisitiza pia kuwa SADC inapaswa kuondoa vikosi vyake (kutoka Afrika Kusini, Tanzania na Malawi) wakisema misheni yao DRC haina uhalali tena.

SADC pamoja na jumuiya nyingine za kikanda na kimataifa zikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), nchi zenye Uchumi mkubwa zaidi duniani (G7) na UN wamelaani vita vinavyoendelea na kutaka mapigano yasitishwe. Wote wanalaani waasi kuteka maeneo ya nchi yaliyo chini ya serikali halali ya DRC.

Rwanda, imekuwa ikisisitiza kuwa kinachoendelea DRC ni tatizo la ndani ya DRC na linatakiwa lisuluhishwe na serikali ya nchi hiyo

ambayo wanadai imeshindwa kufanya hivyo na kuwalazimu M23 kudai haki zao kwa mtutu wa bunduki.

Jumuiya ya kimataifa pia ilipinga vikali mwaka 2012 M23 kuteka maeneo yan chi hiyo ikiwemo Goma na hatua kadhaa kuchukuliwa ikiwemo kushambuliwa kwa M23 japo suluhisho la kisiasa halikupatikana.

Swali gumu katika mgogoro unaondelea sasa ni je, suluhu ya kudumu ya kisiasa itapatikana?

0 Comments:

Post a Comment