Je, Raila kushinda uchaguzi wa Umoja wa Afrika leo?
- Na Laillah Mohammed
- BBC Nairobi
Zimesalia saa chache tu, ambapo bara la Afrika na hususan mgombea kutoka Kenya, Raila Odinga kujua hatima yake ikiwa atakuwa mrithi wa Moussa Faki Mahamat kama mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC)
Uchaguzi unaandaliwa leo Februari 15, katika kikao cha Marais ambacho kinatarajiwa kukamilika Jumapili Februari 16.
Waziri huyo Mkuu wa zamani wa Kenya mwenye umri wa miaka 80 anaingia kwenye kinyang'anyiro kikali dhidi ya Mahmoud Ali Yousuf wa Djibouti na Richad Randrimandrato wa Madagascar.
Daktari Peter Mwencha, ambaye ni mhadhiri wa Diplomasia na Afisa Mkuu wa chama cha wataalamu wa masuala ya kimataifa (IRSK) anasema kibarua kitakuwa kigumu kwa mwanasiasa huyo kutoka eneo la Afrika Mashariki.
"Kenya imefanya kampeni kali katika muda huu wote. Raila amejiwasilisha vyema kwa viongozi muhimu katika maeneo yote ya bara, japo kumekuwa na uungwaji mkono wa kampeni yake miongoni mwa Wakenya. Kilichosalia sasa ni kusubiri uchaguzi ufanyike," alisema Dkt. Mwencha katika mahojiano na BBC.
Huku viongozi hao watatu wakijiandaa kwa kura hiyo ambayo imesubiriwa na wengi barani na hata nje ya bara, tangazo la Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuyataka mataifa wanachama kumuunga mkono mgombea wao aliyekuwa Waziri wa mambo ya kigeni wa Madagascar Richard Randrimandrato, kumezua mjadala mkali miongoni mwa Wakenya ikiwa kura alizotarajia "Baba" kama anavyofahamika nchini Kenya, zitapungua na kumuondolea nafasi ya kumrithi Bwana Mahamat ambaye anaondoka mamlakani baada ya kuhudumu kwa miaka minane.
Balozi Erastus Mwencha ambaye amewahi kuhudumu kama Naibu Mwenyekiti wa Tume ya AUC anasema kwamba tangazo hilo halifai kumtia tumbo joto bwana Odinga.
"Hilo hufanyika kwamba secreate kadha hutoa kauli ya aina hii, kuwahimiza wanachama kufanya uamuzi wa pamoja. Ila, tangazo hilo halina ulazima wa kisheria kufuatwa na wanachama. Kila taifa litaangazia mahitaji yake ya kibinafsi. Na wala hamna adhabu ambayo wataipata," alisema Balozi Mwencha.
Kwa mfano, Tanzania ambayo ni mwanchama wa SADC na vile vile Jumuiya ya Afrika MAshariki EAC, huenda isiangazie suala hilo kwa uzito kwa kwa sababu ya siasa za kikanda kuliko Randrimandrato ambaye nchi yake haina ukaribu na eneo la Afrika Mashariki ilipo Tanzania.
Na alipotangaza rasmi nia yake ya kuwania kiti hicho, viongozi kadhaa kutoka EAC akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan walizuru Nairobi, Kenya kwa mualiko wa Rais William Ruto kama njia ya kutafuta ungwaji mkono kwa Raila Odinga.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa nchini Kenya, wakati huu ni nafasi ya Kenya kwa kuwa Tanzania iliwahi kushikilia nafasi hii kati ya 1989 na 2001 Salim Ahmed Salim alipokuwa katibu Mkuu wa Umoja wa nchi huru za Afrika (OAU).
Aidha ilipotajwa kwamba Rais wa zamani Jakaya Mrisho Kikwete, angewania kiti hicho, alitangaza wazi katika uzinduzi wa ugombea wa Raila kwamba hakuwa na nia ya kuwania kiti hicho.

Raila Odinga, atatakiwa kucheza karata zake vyema hususan katika eneo la Afrika ya Magharibi na Kazkazini ambapo lugha ya Kifaransa inatumika kwa ukubwa.
Kulingana na Mhariri Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Athuman Mtulya, suala hili litakuwa na uzito kiasi katika kinyang'anyiro cha Februari 16, ambapo Muungano wa ECOWAS una idadi kubwa ya mataifa yanayozungumza Kifaransa na huenda wakashawishika.
Japo Randramandrato mwenyewe hajaonekana kama amepiga kampeni kama alivyofanya Odinga, ambaye aliwahi kusafiri hadi Misri kupiga kamepni na pia kukutana na viongozi wengine katika eneo hilo akiwemo Rais Bassirou Diomaye Faye, wote wlaivyokuwa jijini New York Marekani kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa," alisema Mtulya.
Kwa upande mwingine Raila anakabiliwa na kibarua kikali kumkata miguu mpinzani wake kutoka eneo la pembe ya Afrika ambao haipo mbali na Kenya. Mahmoud Ali Youssouph.
Djibouti ambayo inazungumza Kifaransa na Kiarabu, huenda ikatafuta uungwaji mkono kutoka mataifa ya Afrika Kaskazini ambayo mengi yanazungumza Kiarabu.
Baada ya kampeni kuelekea ukingoni macho yote yanaelekezwa kwenye kura itakayopigwa, wengi wananajiuliza jinsi kura hii itakavyopigwa.
Kulingana na Balozi Erastus Mwencha, hatua ya mzunguko wa Uenyekiti wa AUC kati ya majimbo Matano ya Afrika yaani, Afrika Kaskazini, Afrika Magharibi, Afrika ya Kati, Afrika Mashariki na Afrika Kusini ilichukuliwa mnamo 2018, katika kikao cha wajumbe baada ya mazungumzo ya kina kuhusu kila eneo kupata fursa ya uwakilishi katika nyadhifa za juu.
Tangu jumuiya ya AU iwe inafahamika kama OAU, uongozi wa ngazi za juu umekuwa ukishikiliwa na mataifa ya Afrika Magharibi au yale ambayo yanazungumza Kifaransa kama lugha rasmi. Mataifa kama vile Mali,Gabon na Chad yametoa viongozi waliowajibikia majukumu katika ngazi za juu, kwenya OAU/AU.
Huku ikiwa ni fursa ya eneo zima la Afrika Mashariki ambapo mataifa kama vile Sudan, Ethiopia, Djibouti, na Eritrea yanajumuishwa, wagombea wawili kutoka eneo hilo wamejitokeza.
Raila Odinga wa Kenya, Mahmoud Ali Youssouf wa Djibouti watamenyana na Richard Randmadrato wa Madagascar ambaye japo taifa lake lipo katika Jumuiya ya SADC, halipo mbali na pwani ya Afrika kwa upande wa chini Tanzania, kwenye Bahari ya hindi.
Je, kura itapigwa vipi?
Watatu hao wanatarajiwa kushiriki kwenye uchaguzi ambao utapigaji kura utafanyika kwa njia ya siri. Marais wa mataifa wanachama wa AU, ndio watakao kuwa wajumbe maalum wenye uwezo wa kupiga kura.
Kulingana na sheria za Jumuiya ya Afrika, ni mataifa ambayo hayakabiliwi na adhabu yoyote ndio yatakayopata fursa ya kupiga kura. Kwa sababu hiyo, ni mataifa 49 pekee ambayo yana uwezo wa kuamua ni nani atakayemrithi Moussa Fakii kama Mwenyekiti wa tume ya AU.
"Kura itakapopigwa, maafisa wa kusimamia uchaguzi huo, watakusanya kura hizo na kuzihesabu.Kisha atahitajika kuwa na uungwaji mkono wa thelithi mbili ya jumla ya kura zilizopigwa , mgombea ambaye atatangazwa mshindi. Ikiwa hakutakuwa na aliyefikisha kiwango hiki, basi kengele itapigwa na kura kupigwa kwa raundi ya pili, ambapo wagombea wawili wa kwanza wataminyana debeni ten ana kulingana na itifaki za kuhesabu kura zitalia kama hapo awali, na kama mambo yatakataa kukamilisha mahitaji ya jinsi sheria za AU zinasema, kura itapigwa kwa mara ya tatu.Ikiwa katika raundi hii hakuna mshindi wa moja kwa moja, bas ikura ya Naibu Mwenyekiti inaendelea na akipatikana mshindi atashikilia wadhifa huo kwa muda wa miezi sita, ambapo uchaguzi wa Uenyekiti utahitajika kuandaliwa upya.' Alisema Balozi Mwencha.
Wakati wa uchaguzi wa 2017, Balozi Amina Mohammed alipomenyana na Waziri Mkuu wa zamani wa Chad, Moussa Fakii Mahamat, kura hiyo ilipigwa kwa raundi saba na hatimaye kuamuliwa kwa kura moja tu, kati ya mashindi na aliyeshindwa.
Wataalamu wa Diplomasia kama daktari Peter Mwencha kutoka IRSK wanasema kwamba kuangushwa kwa Bi Mohammed ambaye alikuwa Waziri wa mambo ya kigeni wakati huo chini ya uongozi wa Uhuru Kenyatta, alikosa kupata uungwaji mkono kwa sababu ambazo zilikuwa zaidi ya upinzani kati ya mataifa yanayozunga Kiingereza na yale yanayozungumza Kifaransa.
Kipi kitarajiwe ikiwa mshindi atapatikana?
Ikiwa Raila Odinga ataukweya mlima wa AU na kufanikiwa kufika kileleni au mmoja kati ya wapinzani wake wawili wakifanikia na ushindi, basi wata subiri uchaguzi wa Naibu mwenyekiti ambao una wagombea sita kutoka Libya, Algeria na Morrocco kufanyika.
Baada ya hapo wajumbe watawachagua makamishena sita, wawili kutoka majimbo matatu ambayo wakati huu hayajawasilisha mgombea kwenye viti vikuu viwili.
Tume hiyo kwa mujibu wa sheria za AU, inaweza kuhudumu kwa miaka minne na vile vile kuongezewa mingine minne ya kazi kama alivyofanyiwa Moussa Fakii Mahamat ambaye anaondoka baada ya miaka minane kazini.
Na je, ikiwa Raila atarejea nyumbani mikono mitupu?
Mchambuzi wa siasa nchini Kenya, Barack Muluka anasema kwamba Raila atarejea nyumbani na kuendeleza siasa za ndani kama kawaida.
"Kwa sasa kiti chake cha mwenyekiti wa chama cha ODM kinaweka moto na Prof. Peter Anyang' Nyong'o -ambaye ni gavana wa jimbo la Kisumu – kwa muda. Na akipoteza, hana pengine pa kurejea isipokuwa nyumbani kwao."
Alisema Muluka huku akisema kwamba ; " Raila, ndio amekuwa kidonda sugu kwa Rais William Ruto, ambaye kwa sasa amemunga mkono.
Kwa asilimia 100 katika kampeni hii. Ni kwa sababu, hangetaka azimio lake la 2027 kuwa na kizingiti kikibwa na ndio maana amefanya kampeni ya kukata na shoka kumhakishia Raila ushindi.
Na je zimwi la 2017 lililompata Amina litamfuata Raila?
Daktari Peter Mwencha anasema kwamba itakuwa vigumu kutabiri kwa sasa. Ila kulingana na uchambuzi uliochapishwa kwenye magazeti makuu ya nchini Kenya, siasa za wakati huo zilikuwa kali na wengi walihisi kwamba huenda labda, Kenya ingelifikiria kumuangazia Mkenya ambaye tayari alikuwa akihudumu kama Naibu Mwenyekiti wa AUC wakati huo. Ila kwa sasa hayo ni maji yaliyomwagika ambayo hayaweza kuzoleka.
Muluka anasema pia, hadhi ya kimataifa ya Raila Odinga huenda ikampa nafasi bora, mbali na kampeni iliyopigwa kumtafutia uungwaji mkono.
Ila wanavyosema wahenga, kura ni kwa debe, na debe litaamua hatima yake Odinga.
Baada ya kivumbi kutifulia, tutajuwa mbivu na mbichi ikiwa ataibuka kidedea.
ليست هناك تعليقات