Kwanini wanawake wa Kenya hawataki kupata watoto?

Tangu ainukie ukubwani Nelly Naisula Sironka, mwenye umri wa miaka 28 raia wa Kenya, hajawahi kupendelea kuwa na watoto- na sasa amefanya maamuzi yasiofutika ya kuhakikisha hatawahi kupata watoto.
Mwezi Oktoba mwaka jana, alikata kauli na kuamua kuchukua hatua ya kufungwa mirija ya uzazi- na kufunga milele njia ya kuwa mama na kuishi maisha ya kipekee bila mtoto.
''Najihisi niko huru,'' aliiambia BBC, akitafakari chaguo lake akiamini ni njia moja ya kujenga mustakabali bora wa maisha yake.
Kati ya mwaka 2020 na 2023, takribani wanawake 16,000 katika mataifa ya Afrika Mashariki walifunga mirija ya uzazi, kulingana na Wizara ya Afya nchini Kenya.
Hata hivyo, haijulikani idadi hiyo inajumuisha wanawake ambao walikuwa tayari wamepata watoto au la.
Lakini Dkt. Nelly Bosirie, mtaalam wa uzazi nchini Kenya, ameelezea kuwa kiwango na umri wa wanawake wanaochukua hatua ya kufunga kizazi inabadilika kwa kasi nchini Kenya.
''Awali, wanawake waliotaka kufunga kizazi walikuwa ni wale wamebarikiwa na watoto kadhaa,'' anasema.
''Lakini sasa, tunashuhudia wanawake ambao hawana watoto wengi wakipendelea kufunga kizazi''.
Mpango huo unajumuisha kuziba mirija ya uzazi ili kuzuia mayai yasirutubishwe.
Inapendekezwa ifanywe na wanawake ambao wameamua hawataki kujifungua watoto siku zijazo, kwani kugeuza hali hii ni vigumu na mara nyingi haiwezekani.
''Madaktari hawapendekezi kufunga uzazi kwasababu kurejesha hali ya kawaida baada ya operesheni hii ina changamoto chungu nzima,'' anasema Dkt.Bosire.
Ingawa amelelewa kwa familia ambayo ina watoto wengi, Bi Sironka anasema hajawahi kupata shinikizo la kuwa na familia kubwa aina hiyo.
Lakini anamshukuru babake mzazi kwa kumtilia mkazo ajikite zaidi masomoni na kati ya vitabu vingi anavyovisoma vimeandikwa na waandishi mashuhuri kama vile Toni Morrison, Angela Davis, na Bell Hooks, kama ufunuo wake.
''Nilitangamana na simulizi nyingi za maisha ya wanawake ambazo hazikuzungumzia watoto kamwe,'' anasema.
Akaongezea: ''Hapo ndipo nilitambua unaweza kuishi bila kupata mtoto wako.''
Baada ya kusubiri wakati muafaka- na akaweka akiba ya kutosha na kupata ajira iliyompa ruhusa ya likizo- aliamua kufanya operesheni hiyo ya kufunga uzazi.
Ilimgharimu shilingi 30,000 za Kenya au dola 230.
Pia hali ilivyo duniani sasa ilimshinikiza kufanya maamuzi hayo.
''Barani Afrika na Marekani kumeongezeka ufashisti na utawala wa kimamlaka,'' anaiambia BBC.
Kuharakisha kutekeleza maamuzi yake alihofia huenda operesheni hiyo haitakuwepo katika siku za usoni.
''Sina uhakika kule Kenya inakoelekea,'' anasema.
Bi Sironka anasema alitaka kufanya operesheni hiyo akiwa bado anafurahia haki zake.
Alipoelezea familia yake, haikuwashtua kwani alikuwa ameelezea mataminio yake ya kuishi maisha bila ya kuwa na mtoto wake.
Na je kuhusu mahusiano au kuchumbiwa?
''Hilo bado nalifikiria,'' alisema hilo akionesha kutojali.

Lakini Bi Sironka hayuko peke yake.
Ni miongoni mwa wanawake nchini kenya walioamua kuishi maisha bila watoto, wakibadilisha matarajio ya wanawake katika jamii na kukumbatia mustakabali wanaoutaka.
Katika majukwaa ya mitandao, wanawake wengi nchini Kenya wanazungumza wazi kuhusiana na uamuzi wao wa kuishi bila watoto na kufunga uzazi.
Miongoni mwao ni mwanamke mwenye umri wa miaka 34 Muthoni Gutho ambaye amesimulia safari yake ya kufunga uzazi kwa kufunga mirija katika video ya zaidi ya dakika 30 iliyochapishwa kwa mtandao wa Youtube.
''Nadhani tamko langu la kwanza lakusema sitaki kuwa na mtoto nilikuwa na miaka 10,'' anaiambia BBC.
Wakati huo mamangu alikuwa mjamzito, na hapo ndio nilianza kutafakari kuhusu maisha yangu ya baadaye ya uzazi.
''Niliota kuwa na mpenzi na pia burudani lakini sikuwahi kujiona nikiwa na watoto,'' anasema.
Kama vile Sironka, uamuzi wa Gutho ulishinikizwa na ari ya kuishi maisha kulingana na matakwa yake.
Alipoamua kutumia tembe za kupanga uzazi, ambazo zilimpa kichefuchefu, aliamua kutafuta suluhu ya kudumu.
Mara ya kwanza kumuona daktari kuhusu kufunga mirija ya uzazi akiwa na umri wa miaka 23, alikabiliwa na vizuizi tele.
Badala yake Daktari alianza kumpa wosia wa kuwa watoto ni baraka.
Aliniuliza,' Ikitokea nimepata mpenzi anayetaka watoto nitafanyaje?'' aliniuliza.
Daktari huyo alionekana kunichorea picha ya kuwa na mwenza na kunisahau nilikuwa nimekuja kufanya operesheni hiyo, anasema.
Bi Gutho ambaye wakati huo alikuwa na miaka 23 alisema kupuuza na daktari kulimvunja moyo.
Akiwa ametamauka, miongo mmoja baadaye Gutho anafanikiwa kufanya alichokitaka tangu utotoni.
Dkt Bosire anasema changamoto iliyopo kwa sasa katika sekta ya afya ni madaktari kubadilisha mitazamo kuwa mwanamke yeyote anayehitaji huduma hii anapaswa kupatiwa bila kubaguliwa kwani ni haki yake kujiamulia kuhusu afya yake.
''Hali hii pia imefungamana na utamaduni wetu, ambapo watu wanaamini sio kawaida kwa mwanamke kufunga uzazi,'' anasema.
Dkt. Kireki Omanwa, mtaalam wa masuala ya uzazi mjini Nairobi, ameiambia BBC suala la kufunga mirija ya uzazi kwa wanawake ambao hawajapata watoto bado linajadiliwa katika taaluma ya udaktari.'' Imebaki kuwa haijakamilika kikamilifu,'' anasema.
Akiwa na miaka 33 Bi Gutho alienda kwa daktari tofauti, akiwa amejihami na orodha ya kwanini ameamua kufunga uzazi.
Mara hii hakukuwa na vikwazo. Daktari alimuuliza maswali ya kimsingi na kukubali kumfanyia operesheni hiyo.
''Daktari alikuwa mkarimu,'' anasema.
Kwasasa anasema anafurahia maamuzi yake na faraja anayoipata kutoka kwa jamii ya wanamitandao.
''Wanawake wanaweza kuchangia pakubwa ulimwenguni kwa njia nyingi. Sio lazima iwe ni kufungua na kulea mtoto.Ninashukuru kuishi katika karne ambayo maamuzi yako yanaheshimiwa,'' anasema.


No comments