Mwamba Akamatwa Akiwa na Sare za JWTZ
Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu linamshikilia Emmanuel Mapana (24) maarufu kwa jina la Mchambi mkazi wa mtaa wa Sima, Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu kukutwa amevaa sare za Jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ) zenye cheo cha Luteni kinyume cha sheria.
Katika taarifa ya Jeshi hilo iliyotolewa leo kwa waandishi wa Habari na Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Edith Swebe ilieleza kuwa Mapana amekamatwa leo Februari 14, 2025 majira ya saa 6:30 mchana.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa Mapana alikamatwa na kikosi kazi cha kupambana na uhalifu na wahalifu cha jeshi hilo, ambapo wakati anakamatwa alikuwa amevalia sare hizo.
Ilielezwa kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa amevaa sare hizo akiwa na gari aina ya Ractic yenye namba za usajili T.560 DCS ambapo alifanyiwa upekuzi nyumbani kwake na kukutwa na mkanda wa JWTZ na kompyuta mpakato (Laptop) moja.
Aidha Kamanda Swebe katika taarifa hiyo, alieleza kuwa Jeshi hilo lilikuwa likimsaka mtuhumiwa huyo kwa muda mrefu kwa kosa la kujifanya mtumishi wa serikali.
Taarifa ilisema kuwa mtuhumiwa huyo amekutwa na sare hizo, wakati yeye siyo askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
No comments