.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

BBC Nairobi

Waziri Mkuu wa zamani nchini Kenya Raila Odinga ambaye alikuwa mgombea wa uenyekiti wa Tume ya AUC alikubali kushindwa na mgombea mwenza waziri wa mambo ya nje wa Djibouti Mahamoud Ali Youssouf.

Akizungumza na vyombo vya habari Jumamosi jioni baada ya kufanyika kwa uchaguzi huko Addis Ababa, Ethiopia, Odinga alimpongeza Youssouf kwa kuibuka mshindi.

"Ninakubali matokeo ya kura. Kwa hivyo mimi mwenyewe ninakubali kushindwa"

"Wanasema kwamba lazima tuimarishe demokrasia katika bara la Afrika na ninataka tutumie hii kama mfano mwema," Raila alisema.

"Hivyo basi, namtakia mshindani mwenzangu Mahmoud Ali Youssouf kila la kheri. Namtakia mafanikio katika kazi yake".

Raila aliwashukuru wale wote waliompigia kura na ambao hawakumpigia, "kwa sababu wametumia vyema haki zao za kidemokrasia," alisema.

Raila Odinga aliongeza kwamba alikuwa tayari kwa kila hali itakayotokea ama kushinda au kushindwa kabla ya uchaguzi.

"Sina machungu. Nina furaha sana na kama haitoshi, bado ninapatikana kutoa huduma yoyote kwa bara hili katika uwezo mwingine wowote," alisema.


Vile vile, Raila Odinga aliangazia safari yake ya kampeni na kukiri kuwa alisafiri maeneo mengi barani Afrika.

"Nilijitolea kama mgombea, na kwa miezi kadhaa iliyopita nimetembea maeneo mbalimbali kukutana na viongozi, nikiwarai wanipigie kura. Leo wamejieleza na hali ilivyo, ni kwamba hatukufanikiwa", alisema.

Raila alisisitiza hitaji la kuimarisha usawa katika bara hili.

"Ninashukuru sana kwa zoezi la leo. Ninawashukuru watu wa Afrika."

Alipoulizwa na wanahabari nini kinafuata, Raila Odinga alisema "sasa nitarudi nyumbani, kuna mambo mengi ya kufanya".

Pia Bwana Raila alizungumzia changamoto inayoendelea kukabili eneo la Afrika kwa sasa, mzozo wa DR Congo.

"Suala la DRC bado linaendelea kuwa tata. Mateso tunayoshuhudia hayakubaliki kabisa. Watu wasio kuwa na hatia wanauawa, watoto, wanawake na kadhalika. Lazima isitishwe," alisema.

Mgombea kutoka Djibouti Mahamoud Ali Youssouf alipata ushindi baada ya kupata kura 33 katika raundi ya 7 ya upigaji kura ambayo alikuwa mgombea peke yake.

Raila alijiondoa katika raundi ya sita baada ya kushindwa na Youssof katika raundi ya tano na ya sita huku mgombea wa Madagascar Richard Randriamandrato akiondoka kinyang'anyironi mapema baada ya kushika mkia kwenye raundi wa kwanza, pili na tatu.

,

CHANZO CHA PICHA,REUTERS

Katika awamu ya kwanza ya uchaguzi, Raila alipata kura 20, Youssouf 18 na Randriamandrato 10 huku nchi moja ikikosa kupiga kura.

Bwana Raila hakuweza kutangazwa mshindi kwa sababu mgombeaji anahitajika kupata angalau kura 33.

Awamu ya pili, Raila Odinga alipata kura 22, Youssouf 19 na Randriamandrato 7.

Awamu wa tatu, Youssouf alichukua uongozi kwa kura 23, Raila 20 na Randriamandrato kura 5 huku nchi moja ikikosa kupiga kura.

Awamu ya nne, Youssouf alipata kura 25, Raila kura 21 huku kura 1 ikiharibika. Waliokosa kupiga kura ni mataifa mawili 2.

Katika awamu ya tano, Youssouf alipata kura 26 huku Raila akipata 21. Hakuna kura iliyoharibika lakini taifa 1 lilikosa kupiga kura.

Awamu ya sita Youssouf alipata kura 26, Kenya ikipata kura 22. Hakuna kura iliyoharibika huku taifa 1 likikosa kupiga kura.

Na katika awamu ya saba Mohammmed Ali Youssouf wa Djibouti alipata kura 33 na kuibuka mshindi.