Wafahamu wanamgambo 'wanaochochea uhasama' baina ya DRC na Rwanda

Kama umekuwa ukifuatilia mzozo unaoendelea wa DRC, bila shaka umesikia herufi FDLR zikitajwa mara kwa mara hasa Rwanda inapohusika . FDRL ni kifupi cha maneno ya Kifaransa (Forces démocratiques de libération du Rwanda), ikimaanisha, Jeshi la Ukombozi wa Rwanda), linalotuhumiwa na Rwanda kuhatarisha usalama wake na hata kupanga kuung'oa mamlakani utawala wa Kigali.
Licha ya kwamba si mara ya kwanza kwa kundi hili kutajwa katika mzozo wa Kongo, halijawa maarufu sana hapo awali kama sasa kutokana na mzozo wa mashariki mwa Kongo kugubikwa na machafuko yanayotekelezwa na vikundi mbalimbali vya wapiganaji, FDLR wakimwemo.
Hata hivyo katika mzozo unaoendelea, kundi la FDLR limesikika sana hususani katika kauli kali za Rais wa Rwanda Paul Kagame, alipoishutumu serikali ya Kinshasa kuwaunga mkono wapiganaji hao na mamluki ili kuung'oa utawala wake mamlakani.
Lakini Je, FDLR ni akina nani hasa ?

Kundi la FDLR ni kundi linalohusishwa moja kwa moja na mauaji ya kimbari ya Mwaka 1994 yaliyosababisha vifo vya Wanyarwanda takribani milioni moja, wengi wao wakitoka katika jamii ya Watutsi. Wahutu wachache waliokuwa na msimamo wa kati pia waliuawa.
Baadhi ya wafuasi wa kundi hili walikuwa wanajeshi wa zamani wa Rwanda ( X-FAR ) na wanamgambo wa serikali hiyo, maarufu kama Interahamwe waliopigana na vikosi vya Rwandan Partiotic Front (RPF- Inkotanyi), jeshi lililokuwa la wapiganaji wakimbizi wa Rwanda waliokuwa uhamishoni.
Jeshi la RPF ambalo liliongozwa na rais wa sasa wa Rwanda Paul Kagame, lilipata ushindi katika vita hivyo mwaka 1994 na kuwalazimisha wanajeshi wa zamani wa Rwanda na wanamgambo wa Interahamwe kukimbilia katika Zaire (DRC ya sasa), huku baadhi yao wakichangamana na raia wakimbizi na wengine wakijificha katika misitu ya Kongo na kuanzisha uasi na kutekeleza ukatili na mauaji dhidi ya raia wa Kongo na kuwashambulia ndani ya mipaka ya Rwanda.
Mnamo mwaka 2000, kundi la FDLR liliundwa rasmi na baadhi ya wanajeshi hawa wa zamani wa Rwanda, wanamgambo wa Interahamwe pamoja na makundi mengine madogo ya wapiganaji wa Kihutu.
Tangu wakati huo kundi la FDLR limekuwa likitekeleza maasi kama vile ubakaji wa watoto na wanawake pamoja na mauaji ya kikatili ndani ya DRC .
FDLR pia imekuwa ikifaya mashambulizi ndani ya mipaka ya Rwanda, hayo ni pamoja na yale waliyoyafanya katika msitu wa Mbuga ya Wanyama ya Virunga, mwaka 1998 ambapo watu zaidi ya 10 waliuawa katika mji wa Gisenyi uliopo mpakani mwa Rwanda na DRC na yale waliyoyafanya katika wilaya ya Nyaruguru Juni 2018, eneo la Nyungwe, na Wilaya ya Nyamagabe Disemba 2018.
Wafuasi wa kundi hili wamekuwa wakisakwa na mahakama ya kimataifa kwa ajili ya mauaji ya kimbari ya Rwanda kujibu mashtaka ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, huku Marekani ikilitaja kundi hili kuwa la ugaidi kutokana na ukatili na mauji yanayotekelezwa na wafuasi wake.
'FDLR kiini cha mzozo kati ya DRC na Rwanda'

Rwanda mekuwa ikiishutumu serikali ya Kinshasa kushirikiana na kuwaingiza baadhi ya wapiganaji wa FDLR ndani ya jeshi lake la FRDC kwa njama za kuitoa mamlakani serikali ya Rwanda, shutuma ambazo DRC inakanusha.
Ripoti za Monusco, Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu zimekuwa zikiwashutumu wafuasi wa kundi hili kutekeleza mauaji, kupora maliasili za Congo, ubakaji na kuwaingiza watoto jeshini.
Katika ripoti zake kuhusu uhalifu na mauaji DRC, Shikrika la hali za binadamu la Human Rights Watch limelishutumu kundi la FDLR mara kwa mara kwa kutekeleza maasi likiungwa mkono na jeshi la DRC.
Katika ripoti yake mwaka 2022, Human Rights Watch ilisema ''ilipata taarifa za kuaminika kwamba wanajeshi wa Congo kutoka kikosi cha 3411 cha Tokolonga walitoa zaidi ya masanduku kumi na mbili ya risasi kwa wapiganaji wa FDLR huko Kazaroho, moja ya ngome zao katika Hifadhi ya Taifa ya Virunga, Julai 21.
'' Wapiganaji wa FDLR wamewaua mamia ya raia kwa miaka mingi mashariki mwa Kongo, wakati fulani waliwakatakata hadi kufa kwa mapanga au majembe, au kuwachoma majumbani mwao. Wapiganaji hao wamefanya ubakaji usiohesabika na vitendo vingine vya ukatili wa kingono,'' ilielezea ripoti hiyo.
Wenyeji katika Maeneo ya Mashariki mwa DRC wanashutumu jeshi la Kongo kwa kushirikiana nao, na kuwaacha wenyeji wakiishi na kujitafutia riziki hatarini.
"Wakati mmoja, [FDLR] walikuja kuchoma vijiji … zaidi ya nyumba 200," alisema Eric Kambale, kasisi mwanafunzi katika parokia ya Luofu…Watu waliungua ndani. Jeshi la Congo lilikuwa umbali wa kilomita moja wakati hayo yakitokea."
Bwana Kambale anasema watu wa Luofu waliishi chini ya tishio la vita vya mara kwa mara hadi majeshi ya Umoja wa Mataifa yalipodhibiti tena eneo hilo mwaka 2010.


No comments