Zaidi ya wanawake 100 walibakwa na kuchomwa wakiwa hai katika gereza la Dr Congo - UN inasema

Zaidi ya wafungwa 100 wa kike walibakwa na kisha kuchomwa moto wakiwa hai wakati wafungwa walipotoroka jela katika mji wa Goma nchini Congo, kulingana na UN.
Mamia ya wafungwa walitoroka katika gereza la Munzenze Jumatatu iliyopita, baada ya wapiganaji wa kundi la waasi la M23 kuanza kuuteka mji huo.
Kati ya wanawake 165 na 167 walivamiwa na kunyanyaswa na wafungwa wa kiume walipovunja gereza, hati ya ndani ya Umoja wa Mataifa iliyoonekana na BBC inasema.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa wengi wa wanawake hao waliuawa baada ya wafungwa hao kuchoma moto gereza hilo.
BBC haijaweza kuthibitisha ripoti hizo.
Goma, jiji kubwa lenye zaidi ya watu milioni moja, lilitekwa baada ya kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda kuingia na kuteka eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Jiji hilo lilikumbwa na machafuko, huku miili ikiwa imetapakaa mitaani na makombora yakiripotiwa kuonekana juu ya nyumba za makazi.
Picha za jela kuvunjwa za wiki iliyopita zilionyesha watu wakitoroka kutoka kwa jengo hilo huku moshi ukiendelea kupaa kwa nyuma.
Milio ya risasi pia ilisikika.
Katika video tofauti, watu wanaoaminika kuwa wafungwa waliotoroka, walionekana wakiwa wamewasili katika mitaa ya Goma.
Zaidi ya watu 2,000 waliuawa wakati waasi wa M23 wakikabiliana na wanajeshi wa Congo na washirika wao, serikali ya DR Congo imesema.
Umoja wa Mataifa unasema takriban watu 900 waliuawa na karibu 3,000 kujeruhiwa.
Haikuwa wazi kwa nini idadi ya vifo vya Umoja wa Mataifa na DR Congo inatofautiana.


No comments