Watoto Milioni 1 wenye utapiamlo hatarini kupoteza maisha Afrika

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limesema Ijumaa kwamba litaishiwa na chakula cha dharura cha kuokoa maisha ya watoto wanaougua utapiamlo mkali katika nchi za Afrika ndani ya miezi miwili ijayo kutokana na ukosefu wa ufadhili, hali iliyoathirishwa zaidi na hatua ya utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani kupunguza misaada ya kigeni.
Kwa mujibu wa UNICEF, takriban watoto 1.3 milioni walio na umri wa chini ya miaka mitano wanaougua utapiamlo mkali wako katika hatari ya kupoteza msaada muhimu wa kuokoa maisha yao mwaka huu nchini Ethiopia na Nigeria.
"Bila ufadhili mpya, tutakosa chakula cha dharura cha Ready-to-Use Therapeutic Food (RUTF) kufikia Mei, na hiyo inamaanisha kuwa watoto 70,000 nchini Ethiopia wanaotegemea matibabu haya hawataweza kuhudumiwa," alisema Kitty Van der Heijden, naibu mkurugenzi mtendaji wa UNICEF, alipoongea na waandishi wa habari mjini Geneva kwa njia ya video kutoka Abuja, Nigeria.
Nchini Nigeria, UNICEF inasema huenda ikaishiwa na chakula cha msaada kwa watoto 80,000 wenye utapiamlo kufikia mwishoni mwa mwezi huu. Van der Heijden alieleza kuwa alitembelea hospitali moja mjini Maiduguri ambako alimkuta mtoto aliyekuwa na utapiamlo mkali kiasi kwamba ngozi yake ilikuwa inatoka.
Katika miaka ya hivi karibuni, wahisani wa kimataifa wamepunguza michango yao kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa, ikiwemo UNICEF. Changamoto ya ufadhili ilizidi kuwa mbaya baada ya Marekani, ambayo ni mfadhili wake mkubwa, kusitisha kwa siku 90 misaada yote ya kigeni mnamo siku ya kwanza ya Rais Donald Trump kurejea Ikulu ya White House Januari mwaka huu.
Download/Pakua/Install App ya Abedijr kupitia google crome Bofya Hapa
app hii aipatikani google playstore ka sasa hupatikana kwenye wavuti yetu hii



No comments