Makumi ya wahamiaji wa Afrika wauawa katika shambulio la Marekani dhidi ya Wahouthi

Takriban wahamiaji 68 wa Afrika wameuawa katika shambulizi la anga la Marekani dhidi ya kituo kimoja kinachodhibitiwa na Wahouthi kaskazini-magharibi mwa Yemen, kituo cha televisheni cha kundi hilo lenye silaha kimesema.
Al Masirah iliripoti kuwa wahamiaji wengine 47 walijeruhiwa, wengi wao wakiwa vibaya sana, wakati kituo hicho katika jimbo la Saada kikilipuliwa kwa bomu.
Kituo hicho kilichapisha picha zinazoonyesha miili mingi iliyofunikwa kwenye vifusi vya jengo lililoharibiwa.
Hakukuwa na maoni ya mara moja kutoka kwa jeshi la Marekani.
Lakini shambulio hili lilijiri saa chache baada ya Kamandi Kuu ya Marekani kutangaza kwamba vikosi vyake vimepiga shabaha zaidi ya 800 tangu Rais Donald Trump kuamuru kuimarishwa kwa kampeni ya anga dhidi ya Wahouthi tarehe 15 Machi.
Ilisema mashambulizi hayo "yameua mamia ya wapiganaji wa Houthi na viongozi wengi wa Houthi", wakiwemo maafisa wakuu waliokuwa wakisimamia mipango ya makombora na ndege zisizo na rubani.
Mamlaka zinazoongozwa na Houthi zimesema shambulio hilo limesababisha vifo vya makumi ya raia, lakini wameripoti majeruhi wachache miongoni mwa wanachama wa kundi hilo.
Kituo cha wahamiaji huko Saada kiliripotiwa kuwa na Waafrika 115 wakati kiliposhambuliwa Jumapili usiku.
Licha ya mgogoro wa kibinadamu nchini Yemen uliosababishwa na mzozo wa miaka 11, wahamiaji wanaendelea kuwasili nchini kwa boti kutoka Pembe ya Afrika, wengi wao wakiwa na nia ya kuvuka hadi katika nchi jirani ya Saudi Arabia kutafuta kazi.
Badala yake, wanakabiliwa na unyanyasaji, kuwekwa kizuizini, ghasia, na safari hatari kupitia maeneo yenye migogoro, kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM).
Mwaka 2024 pekee, inasema, karibu wahamiaji 60,900 waliwasili nchini, bila njia ya kuishi.
Mapema mwezi huu, serikali inayoongozwa na Houthi ilisema mfululizo wa mashambulizi ya anga ya Marekani kwenye kituo cha mafuta cha Ras Isa kwenye pwani ya Bahari Nyekundu yaliwauwa watu wasiopungua 74 na wengine 171 kujeruhiwa.
Ilisema kituo hicho ni kituo cha kiraia na kwamba mashambulizi hayo yalijumuisha "uhalifu wa kivita".
Centcom kilisema shambulio hilo liliharibu uwezo wa Ras Isa kupokea mafuta na kwamba "litaanza kuathiri uwezo wa Houthi sio tu kufanya operesheni, lakini pia kupata mapato ya mamilioni ya dola kwa shughuli zao za kigaidi".
Download/Pakua/Install App ya Abedijr kupitia google crome Bofya Hapa
app hii aipatikani google playstore ka sasa hupatikana kwenye wavuti yetu hii


No comments