Mahakama Kuu Tanzania yatupilia mbali kesi ya kudharau amri ya mahakama dhidi ya viongozi wa CHADEMA

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, imetupilia mbali shauri la kudai kukiukwa kwa amri ya mahakama lililowasilishwa dhidi ya viongozi wa chama cha upinzani CHADEMA.
Kesi hiyo, iliyosajiliwa kwa namba 24850 ya mwaka 2025, ilifunguliwa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Saidi Issa Mohammed, na wenzake, wakiiomba mahakama kutoa amri ya kuwakamata na kuwaweka gerezani baadhi ya viongozi waandamizi wa chama hicho cha upinzani nchini Tanzania, akiwemo Makamu Mwenyekiti John Heche.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Awamu Mbagwa, ambaye alikubaliana na hoja za wakili wa utetezi, Hekima Mwasipu, kwamba maombi hayo yaliwasilishwa nje ya muda kisheria na hivyo hayakuwa na mashiko ya kuendelea kusikilizwa.
Akizungumza nje ya mahakama baada ya uamuzi huo, wakili Mwasipu alisema:
“Uamuzi wa leo ni hatua muhimu ya mwanzo. Tangu Juni 10, 2025, kesi hii ilizuia shughuli zote za CHADEMA nchini kutokana na tafsiri potofu ya zuio lililotolewa baadaye dhidi ya Katibu Mkuu. Kwa kuwa shauri hili lilianzishwa kwa malengo ya kukwamisha harakati za chama, ni muhimu sasa waliolianzisha watumie utaratibu huohuo kuliondoa kabisa mahakamani ili CHADEMA ipate haki na uhuru wake wa kikatiba, ikiwemo kufanya vikao vyake kwa uwazi na kutathmini matukio yaliyoikumba nchi.”
Mwasipu alirejea pia maafa yaliyoripotiwa kutokea Oktoba 29, akidai kuwa serikali haijatoa takwimu kamili kuhusu kile alichokitaja kama “ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu”.
Alishtumu kile alichokiita “ukwepaji wa uwazi” na akazitaka mamlaka kutoa taarifa rasmi kwa umma.
Hata hivyo, maelezo hayo bado hayajathibitishwa na vyombo huru, na serikali imekanusha madai hayo katika matamko ya awali.
Uamuzi wa mahakama leo unatarajiwa kufungua njia ya kurejea kwa baadhi ya shughuli za chama zilizokuwa zimekwamishwa na shauri hilo kwa miezi kadhaa.
Download/Pakua/Install App ya Abedijr kupitia google crome Bofya Hapa
app hii aipatikani google playstore kwa sasa hupatikana kwenye wavuti yetu hii


No comments