Rais wa Nigeria Atangaza Hali ya Dharura ya Usalama Baada ya Wimbi la Mashambulizi

Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, ametangaza hali ya dharura ya usalama baada ya ongezeko kubwa la mashambulizi ya kigaidi na utekaji watu katika baadhi ya majimbo nchini. Akitangaza hatua hiyo Jumatano, Novemba 26, 2025, Tinubu alisema serikali haitavumilia “mawakala wa uovu” wanaoihujumu nchi.
Katika agizo lake, Rais ameamuru kuongezwa kwa askari 20,000 wa polisi, na hivyo kufikia lengo la askari 50,000 litakalosaidia kufunika maeneo yenye hatari zaidi. Vilevile, kambi za NYSC zitatumika kwa muda kama vituo vya mafunzo ili kuongeza kasi ya kupeleka maafisa wapya kwenye maeneo yenye changamoto za kiusalama.
Tinubu pia ameagiza maafisa wa polisi waliokuwa wakilinda watu maarufu (VIPs) kurudishwa na kufanyiwa mafunzo ya dharura kabla ya kupelekwa kupambana na ugaidi na utekaji.
Rais amesema Idara ya Usalama wa Taifa imepata ruhusa ya kupeleka walinzi wa misitu (forest guards) waliomaliza mafunzo ili kukabiliana na magaidi na majambazi wanaojificha maeneo ya porini, huku ajira zaidi zikitarajiwa kutolewa kwa ajili ya umoja huo wa kiusalama.
Amesisitiza kuwa operesheni za kuwaokoa wanafunzi wa St. Mary’s Catholic School waliotekwa katika Jimbo la Niger, pamoja na raia wengine waliotekwa, zitaendelea bila kukoma.
Katika hatua nyingine, Tinubu ameitaka Bunge la Nigeria kuanza mchakato wa kurekebisha sheria ili kuruhusu uundwaji wa polisi wa majimbo (state police) kwa maeneo yanayotaka mfumo huo—hoja ambayo imejadiliwa kwa miaka mingi kutokana na kuongezeka kwa vitisho vya usalama.
Aidha, amewaonya viongozi wa serikali za mitaa kuepuka kufungua shule za bweni katika maeneo ya mbali bila usalama wa kutosha, na kuzitaka makanisa na misikiti kuongeza ulinzi hasa katika maeneo hatarishi ili kulinda jamii.
Download/Pakua/Install App ya Abedijr kupitia google crome Bofya Hapa
app hii aipatikani google playstore kwa sasa hupatikana kwenye wavuti yetu hii


No comments