Na. Sophia Kingimali.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angella Kairuki, ametoa wito kwa wizara na taasisi zote za serikali kuharakisha matumizi ya mifumo ya kidijitali, hususan mfumo wa anwani za makazi, ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuchochea uchumi wa kidijitali nchini.
Akizungumza leo Januari 8, 2026, katika kilele cha Wiki ya Anwani za Makazi na Maonyesho ya Teknolojia ya Posta yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Waziri Kairuki amesema mfumo huo ni nguzo muhimu katika kutambua makazi ya wananchi na kurahisisha utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi.
Waziri Kairuki amesema serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano kwa lengo la kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kidijitali unaozingatia ubunifu, teknolojia na maarifa.
Amebainisha kuwa hadi sasa jumla ya anwani za makazi takribani milioni 12.9 zimeshasajiliwa nchini, huku mifumo 29 kutoka taasisi 23 za serikali na sekta binafsi ikiunganishwa na mfumo huo.
Ameongeza kuwa mfumo huo umeonesha manufaa katika sekta za elimu, fedha, usalama na huduma za dharura, ambapo taasisi kama Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na Jeshi la Zimamoto zimeanza kuutumia kuboresha huduma.
Waziri Kairuki amesema kupitia mfumo huo, serikali imeweza pia kusaidia wananchi wakati wa majanga kwa kutambua kaya zilizoathirika na kufikisha misaada kwa haraka.
Amewahimiza wadau wa sekta binafsi, wakiwemo benki na kampuni za mawasiliano, kuutumia mfumo huo katika kutambua wateja wao ili kuongeza ujumuishi wa kifedha.
Katika hafla hiyo, Wizara ya Mawasiliano ilikabidhi vishikwambi zaidi ya 5,000 kwa watendaji wa mitaa, kata na vijiji ili kuwawezesha kusasisha taarifa za makazi kwa wakati.
Waziri amesema lengo la serikali ni kuhakikisha watendaji wote, kuanzia ngazi ya taifa hadi vijijini, wanakuwa na vitendea kazi vya kisasa ili mfumo huo utoe taarifa sahihi muda wote.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Hamis Abdullah, amesema mfumo wa anwani za makazi unapatikana kupitia tovuti na programu ya NAPA na umeongeza matumizi kwa zaidi ya asilimia 70 ndani ya mwaka mmoja.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hassan Juma, amesema Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha mfumo huo unatekelezwa kikamilifu ili kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi.

Download/Pakua/Install App ya Abedijr kupitia google crome Bofya Hapa
app hii aipatikani google playstore kwa sasa hupatikana kwenye wavuti yetu hii

0 Comments:
Post a Comment