Hamas yawaachia huru mateka sita wa Israel
Mateka wa sita aliyeachiwa mwishoni alifahamikwa kwa jina la Hisham al-Sayed (37) pia baadaye alikabidhiwa kwa Shirika la Msalaba Mwekundu. Hisham alikuwa akishikiliwa mateka na Hamas kwa zaidi ya miaka 10. Israel itatakiwa pia kuwaachilia mamia ya wafungwa wa Kipalestina wanaokadiriwa kufikia idadi ya 600.
Soma pia: Makabidhiano ya miili ya mateka wa Israel yakosolewa
Mabadilishano hayo ya mateka na wafungwa ni sehemu ya makubaliano ya usitishwaji mapigano huko Gaza. Hamas imesema Jumamosi kuwa iko tayari kutekeleza awamu ya pili ya mpango wa makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza, awamu ambayo itatakiwa kuendeleza hatua za kubadilishana mateka na wafungwa na kusitisha kabisa vita huko Gaza huku vikosi vya Israel vikijiondoa kabisa katika Ukanda huo.
Israel: Mwili wa mateka uliokabidhiwa ni wa Shiri Bibas
Israel imethibitisha siku ya Jumamosi kuwa mwili uliokabidhiwa jana na kundi la Hamas ni wa mateka mwanamke Shiri Bibas na hivyo kumaliza hali ya mkanganyiko.
Siku ya Ijumaa, Waziri Mkuu wa IsraelBenjamin Netanyahu aliilaumu Hamas kwa kushindwa kukabidhi mwili wa mwanamke huyo aliyetekwa nyara na kundi hilo na kuahidi kuchukua hatua kali.
Siku ya Ijumaa, huzuni ilitawala huko Israel baada ya jeshi kutangaza kuwa mmoja wa miili iliyorejeshwa na Hamas siku ya Alhamisi haukuwa wa bi Shiri Bibas, mama wa watoto wawili wadogo waliokuwa wakihofiwa kufariki kwa muda mrefu.
"Jumamosi asubuhi tulipokea habari tulizoziogopa zaidi. Shiri wetu aliuawa akiwa kifungoni na sasa amerejea nyumbani kwa wanawe, mume, dada yake na familia yake yote kupumzika. Licha ya hofu yetu juu ya hatima yao, tuliendelea kutumaini kwamba tungewakumbatia, lakini sasa tuna uchungu na huzuni," alisema mwanafamilia.
Familia ya Bibas, akiwemo mume wake Yarden Bibas, na watoto wao Ariel (4) na Kfir (miezi 9), wamekuwa ishara yenye nguvu inayodhihirisha majonzi makubwa ya kitaifa kufuatia shambulio baya la Hamas dhidi ya Israel Oktoba 7, 2023.
No comments