Kwa nini saratani ya mapafu inaongezeka kwa wanawake ambao hawajawahi kuvuta sigara?

- Pinar Uysal-Onganer
- BBC
Visa vya saratani ya mapafu vinaongezeka kwa watu ambao hawajawahi kuvuta sigara, haswa miongoni mwa wanawake, kulingana na utafiti mpya wa taasisi ya saratani ya Shirika la Afya Duniani (WHO).
Matokeo hayo, yamechapishwa katika jarida la The Lancet Respiratory Medicine, yanaonyesha saratani ya adenocarcinoma, aina ya saratani ya mapafu kwa watu wasiovuta sigara, inachukua karibu 60% ya kesi za ugonjwa huo kwa wanawake, ikilinganishwa na 45% kwa wanaume.
Takriban visa vipya milioni 2.5 vya saratani ya mapafu viligunduliwa duniani kote mwaka 2022 - ongezeko la visa 300,000 tangu 2020.
Sababu ni nini?

Utafiti unasema sababu za kimazingira, hasa uchafuzi wa hewa, jeni na mfumo wa kinga ya mwili, ndio sababu ya ongezeko hili la saratani ya mapafu isiyohusiana na sigara.
Mojawapo ya sababu kuu ya saratani ya mapafu kwa wasiovuta ni mabadiliko ya kijeni, haswa mabadiliko katika jeni ya EGFR. Jeni hii hutoa maagizo ya kutengenezwa protini kwenye seli zinazohusika katika ukuaji na mgawanyiko.
Mabadiliko katika jeni hii husababisha mgawanyiko wa seli usiodhibitika na ukuaji wa saratani. Kansa hii iko 50% kwa wanawake wa Asia wasiovuta sigara, na 19% kwa wanawake wa Magharibi wasiovuta sigara, ikilinganishwa na 10-20% kwa wanaume wasiovuta sigara katika maeneo hayo.
Maendeleo katika upimaji wa (jeni) vinasaba yamerahisisha kugundua mabadiliko haya. Hata hivyo, kuongezeka kwa uchafuzi wa hewa, kunajuulikana kusababisha mabadiliko katika jeni ya EGFR.
Mabadiliko mengine ya kijeni ambayo huchochea ukuaji wa uvimbe wa saratani ni pamoja na mabadiliko katika jeni ya ALK na ROS1. Ni takribani asilimia 5 ya visa vya saratani ya mapafu kwa wasiovuta sigara husababishwa na mabadiliko hayo.
Mabadiliko haya ya jeni yanaonekana zaidi kwa wanawake vijana wasiovuta sigara, haswa barani Asia. Kwa bahati nzuri, mipango iliyoboreshwa ya uchunguzi, haswa katika nchi za Asia Mashariki, husaidia kugundua mabadiliko haya mara kwa mara.
Mabadiliko ya jeni TP53, ambayo ni muhimu katika kuzuia uvimbe, pia yanaonekana kupatikana zaidi kwa wanawake wasiovuta sigara kuliko wanaume. Jeni hii huzuia seli kuwa na saratani, na mabadiliko yake husababisha ukuaji wa seli usiodhibitika. Homoni ya estrojeni inaweza kuungana na TP53 iliyobadilika, na kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya mapafu kwa wanawake.
Jeni nyingine ni ya KRAS. Mabadiliko katika jeni hii mara nyingi huhusishwa na saratani ya mapafu inayohusiana na sigara. Lakini mabadiliko yake yanawakumba wasiovuta sigara, hasa wanawake na kusababisha saratani.
Tafiti zinasema chembe ndogo ndogo zinazopeperuka hewani, au kwa jina la kitaalamu PM2.5 (ambazo ni ndogo mikromita 2.5 au ndogo zaidi), ni sababu ya mabadiliko haya kwa wanawake wasiovuta sigara.
Viwango vya PM2.5 vinaendelea kuongezeka katika miji mingi, chembe hizi zinaelezwa kuwa ndio sababu inayochangia sio tu saratani ya mapafu, lakini pia aina zingine za saratani kwa wanawake.
Mbali na mabadiliko ya jeni, mabadiliko ya homoni kuchangia ukuaji wa saratani kwa wanawake vilevile.
Kinga kushambulia seli

Mbali na chembe za urithi (jeni) na homoni, uvimbe wa muda mrefu unaweza pia kuchangia saratani ya mapafu kuongezeka kwa wanawake wasiovuta sigara.
Wanawake wana uwezekano mkubwa wa kupata tatizo la kinga ya mwili kushambulia seli zenye afya (autoimmune), shida hiyo ya mfumo wa kinga inaweza kuchangia saratani. Kinga kushambulia tishu zenye afya kunasababisha uharibifu wa tishu wa mara kwa mara, na kusababisha mabadiliko katika DNA na kukuza ukuaji usio wa kawaida wa seli, mambo ambayo huongeza hatari ya saratani.
Magonjwa ya kinga kushambulia seli yamekuwa yakiongezeka ulimwenguni kote, ikielezwa sababu ni pamoja na mabadiliko ya mazingira, mabadiliko ya lishe na mabadiliko ya vijidudu wanaoishi kwenye matumbo yetu ambao wana jukumu muhimu katika afya yetu.
Zaidi ya hayo, mambo kama vile uchafuzi wa mazingira, kemikali za nyumbani, na mambo yanayohusiana na kazi huzidisha matatizo ya mfumo wa kinga, na kuongeza hatari ya saratani.
Uchafuzi wa hewa kwa muda mrefu umeelezwa kuwa chanzo cha hatari kwa saratani ya mapafu. Na ushahidi huu mpya unaonyesha wanawake wako hatarini zaidi
Mazingira na maumbile

Uchunguzi unaonyesha muundo wa mapafu ya wanawake na utendaji kazi huwafanya wawe rahisi kuathiriwa na madhara ya uchafuzi wa mazingira.
Mapafu ya wanawake ni madogo kuliko ya wanaume, yana njia nyembamba za hewa, ambazo zinaweza kusababisha chembe ndogo zaidi, kama vile PM2.5, kunasa kwenye mapafu yao.
Wakati wanaume mara nyingi wanakabiliwa na uchafu wa mazingira kutokana na kazi za viwandani, wanawake hutumia muda mwingi ndani ya nyumba, ambapo huvuta moshi wenye sumu wakati kupikia na kupasha moto.
Uchafuzi wa hewa, kama vile kuni, makaa ya mawe na mafuta ya taa, huongeza hatari ya saratani ya mapafu. Wanawake wanaofanya kazi katika maeneo kama vile viwanda vya nguo, saluni na hospitali pia huathirika zaidi na kemikali hatari zinazoweza kuharibu mapafu yao.
Katika miji inayopanuka kwa kasi, wanawake mara nyingi wako katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa magari na uchafuzi wa viwanda.
No comments