Mwanablogu wa Rwanda Aimable Karasira ajitetea mahakamani

Mahakama inayoshughulikia kesi za uhalifu wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda imeanza kusikiliza utetezi wa mwanablogu ambaye pia ni mhadhiri wa zamani wa chuo kikuu Aimable Karasira.
Ni wiki chache baada ya mshtakiwa kulikataa jopo la majaji kwa madai ya kutomtendea haki kisheria,lakini jopo likakataa kubadilishwa.
Karasira ameshitakiwa kwa makosa 6 yakiwemo kukana mauaji ya kimbari,kueneza uvumi kwa lengo kusababisha vurugu miongoni mwa wanyarwanda na kutotaja chanzo cha mali yake akikanusha makosa yote dhidi yake.
Hoja ya Karasira na mawakili wake ilikuwa kwamba mashtaka manne kati ya sita yana uhusiano na kilichosemwa kwenye vyombo vya habari na uhuru wa kutoa maoni hivyo ni lazima kwanza mashtaka hayo kujadiliwa katika ngazi ya chombo kinachosimamia waandishi wa habari RMC .
Hata hivyo, mawakili wa mshtakiwa wamebainisha kuwa mwendeshamashtaka siyo mtaalamu wa maswala ya uandishi wa habari kiasi kwamba ataelewa kwa kina kile kinachozungumzwa katika vyombo vya habari na ikiwa ni sehemu ya uhalifu au la.
Karasira alishtakiwa kufanya mijadala kwenye tovuti ya Youtube inayolenga kupinga mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi.
Akifika mahakamani leo amebainisha kwamba yeye mwenyewe ni muathiriwa wa mauaji hayo.
Mahakamani imechezwa kipande kimoja cha video ambapo mwendeshamashtaka alitoa hoja kwamba mshtakiwa alisema kuwa serikali ya hayati rais Habyarimana ilifanya mauaji ya kimbari ili kujihami dhidi ya watutsi waliounda jeshi la RPF ili kuipiga vita.
Wakizungumzia kuhusu yaliyomo katika kipande hicho cha video Karasira na mawakili wake walisema kauli yake ilitafsiriwa visivyo na mwendesha mashtaka.
Aimable Karasira msanii na mwalimu wa zamani wa chuo kikuu cha Rwanda ambaye anasema ni mwanaharakati alijipatia umaarufu kwenye mtandao wa Youtube kutokana na mijadala yake baadhi waliyoona kuwa ya kukosoa baadhi ya sera za serikali.


No comments