Subscribe Us

Breaking News

SIMBA KWENYE KIBARUA MBELE YA NAMUNGO


CHINI ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids kikosi cha Simba leo kinatarajiwa kuwa kwenye kibarua kizito mbele ya Namungo FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Majaliwa.

Ni mchezo wa mzunguko wa pili kwa wababe hawa kukutana uwanjani katika msako wa pointi tatu ambapo ule wa kwanza uliochezwa Uwanja wa KMC, Complex Simba ilikomba pointi tatu mazima.

Kwenye mchezo wa leo huenda kiungo mshambuliaji Kibu Dennis akaanza baada ya kuwa nje kwa muda wa dakika 180 kwa kuwa alipata maumivu kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Tabora United.

Katika mchezo huo Simba ilipata ushindi wa mabao 3-0 na kusepa na pointi tatu ugenini lakini Kibu hakukomba dakika zote 90.

Ipo wazi kwamba Namungo imekuwa ikitoa ushindani mkubwa kwenye mechi zake dhidi ya Simba hasa ikiwa Uwanja wa Majaliwa jambo ambalo linaongeza ugumu kwa Simba na Namungo kwenye kupata pointi tatu muhimu.

Kocha Mkuu wa Simba ameweka wazi kuwa wanaheshimu wapinzani wao na wataingia kwa tahadhari kubwa katika kusaka pointi tatu muhimu.

“Tunatambua ni mchezo mgumu na timu ambayo tunakutana nayo imekuwa ikipata matokeo hasa nyumbani hivyo tupo tayari na wachezaji watapambana kwa ajili ya kupata pointi tatu muhimu.”

Simba ni namba mbili kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 18 ndani ya msimu wa 2024/25 ikiwa imekusanya pointi 47 inakutana na Namungo yenye pointi 21 nafasi ya 12.

No comments