Subscribe Us

Breaking News

Uchambuzi: Vita vya Mashariki ya Congo vyachochea habari za uongo

 

.
Maelezo ya picha,Wapiganaji wa kundi la M23

Kutekwa kwa mji wa Goma na maeneo jirani na kundi la waasi la M23 kulisababisha kuibuka kwa taarifa potofu. Wakati DR Congo na Rwanda zikitupiana shutuma, watumiaji wa mitandao ya kijamii walikuwa wakizusha madai ambayo hayajathibitishwa.

Madai ambayo yalizidisha hali ya wasiwasi katika eneo ambalo tayari limeharibiwa na miongo kadhaa ya vita na ukosefu wa utulivu.

Utafiti wa BBC uligundua kuwa majukwaa ya mitandao ya kijamii yamekuwa uwanja wa mapambano ya simulizi. Akaunti zenye ushawishi zinazohusishwa na vikundi vya kisiasa zilisambaza picha na video za uongo ili kusukuma mbele ajenda zao, kuleta mkanganyiko miongoni mwa jamii za wenyeji na waangalizi wa kimataifa.

Taarifa potofu zilipata nguvu kutokana na ukimya kutoka katika vyombo vya habari na ukosefu wa taarifa rasmi kutoka serikali ya Congo katika saa za awali za waasi kuingia Goma.

Vyombo vya habari vya ndani, ambavyo mara nyingi viko chini ya shinikizo la kisiasa na ukosefu wa rasilimali za kutosha, kwa kiasi kikubwa vimejizuia kuripoti kusonga mbele kwa M23.

Kujizuia huku, kumeleta ombwe la taarifa, na kuwaacha wananchi na wadau wengine bila taarifa za uhakika za matukio yanayoendelea.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ilikiri kwamba waasi wameuteka mji wa Goma saa 24 baada ya waasi hao kusema. Wakiungwa mkono na wanajeshi wa Rwanda, waasi walisonga mbele hadi katikati ya jiji.


Gavana wa Kivu Kaskazini hajauawa

Vita vya mwanzo vya taarifa vilimuhusu gavana wa kijeshi aliyefariki wa Mkoa wa Kivu Kusini, Meja Peter Cirimwani, ambaye kifo chake kilizua taarifa, kabla ya kuthibitishwa tarehe Januari 27, kwamba aliuawa katika vita na waasi kwenye viunga vya Goma.

Akaunti zinazounga mkono serikali ya Congo zilikanusha kwanza madai ya M23 kwamba Cirimwani aliuawa wakati wa mapigano. Akaunti hizo zilielezea madai hayo kama "propaganda za Rwanda za mtandaoni" zinazolenga kueneza hofu na kukatisha tamaa majeshi ya Congo.

Lakini Rais Félix Tshisekedi baadaye alithibitisha kifo cha Cirimwani na kumteua Meja Jenerali Somo Kakule Evariste kama gavana mpya wa kijeshi wa Kivu Kaskazini.

Vikosi vya serikali vyadhibiti Goma

.

CHANZO CHA PICHA,MONUSCO

Baadhi ya taarifa potofu mtandaoni zilitokana na simulizi za serikali ya Congo, zikiwemo taarifa kuwa vikosi tiifu vya serikali vimedhibiti wilaya zote 18 za mji wa Goma.

Madai haya yalichapishwa sana na akaunti zinazoiunga mkono serikali kwenye mitandao ya kijamii, na kutoa picha yenye matumaini mbali na hali halisi ardhini.

Picha na video zilizotolewa na waandishi huru wa habari na vyanzo vinavyounga mkono M23, zilionyesha hali tofauti na madai ya serikali ya Congo. Picha na video hizo, zinaonyesha udhibiti wa waasi katika vitongoji kadhaa, haswa katika sehemu za magharibi za Goma.

Maeneo muhimu ya kimkakati, ikijumuisha studio za RTNC zinazomilikiwa na serikali karibu na mwambao wa Ziwa Kivu na mlima wa Goma ulionyeshwa kuwa chini ya uvamizi wa waasi tarehe 27 Januari.

Mlima Goma, haswa, ni mahali pazuri pa kusimama ni kuona sehemu kubwa ya magharibi mwa jiji, mlima ambao umeipata M23 faida ya kimbinu.

Ripoti za kweli pia zilisema kuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Goma uliangukia mikononi mwa waasi, lakini ya serikali kukanusha bila kutoa ushahidi.

Ripoti za vyombo vya habari tarehe 29 Januari zilithibitisha kwamba wanajeshi wa Rwanda na wapiganaji wa M23 wanahikilia "karibu maeneo yote ya kimkakati ya Goma."

Kumuua msemaji wa M23

Kinshasa ilisisitiza kwamba vikosi vyake tiifu vinashikilia udhibiti wa mji wa Goma, huku kukiwa na ushahidi wa video zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii ukionesha uongozi wa M23, ukiongozwa na msemaji wa kundi hilo Willy Ngoma, ukiingia Goma.

Akiwa amevalia nguo za kijeshi na pembeni yake akiwa na waasi wenye silaha, Ngoma alionekana akiwahutubia wapiganaji na wafuasi, akieleza taarifa za ushindi wa M23. Pia alipigwa picha tarehe 28 Januari nje uwanja wa ndege wa Goma na kukinzana na taarifa kwamba jeshi la Congo lilimuua.

Ngoma, ambaye yuko chini ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya na Marekani kwa kuhusika kwake katika mzozo huo, amekuwa katika nafasi ya usemaji kwa muda mrefu.

Uwepo wake huko Goma umeimarisha nguvu ya kundi hilo na kupinga madai ya serikali ya Congo kwamba bado inadhibiti Goma.

Kamanda wa waasi yuko hospitalini

Kulikuwa na taarifa kwamba kiongozi wa sasa wa M23, kamanda wa kijeshi, Sultani Makenga, mtu ambaye mara nyingi anajulikana kwa shughuli za kimkakati za kikundi, kwamba yupo hospitalini.

Kukosekana kwa Makenga kulichochea uvumi kwenye mitandao ya kijamii kwamba alipigwa risasi wakati wa mapigano ya hivi karibuni na alikuwa katika hali mbaya katika hospitali ya Kigali, Rwanda.

Hapo awali Makenga alipigwa picha akiwa pamoja na Corneille Nangaa, kiongozi wa kisiasa wa Congo River Alliance (AFC), muungano wa makundi ya waasi na upinzani ambao mshirika wao mkuu ni M23.

Kamanda huyo wa waasi mara ya mwisho alionekana hadharani katika video iliyotolewa na M23 tarehe 25 Januari, wakati wapiganaji wake wakikaribia Goma.

Hakujawa na uthibitisho iwapo Makenga alijeruhiwa na kupokea matibabu Rwanda au yuko hai huko Kaskazini ya Kivu.

Nangaa pia alizungumziwa katika taarifa za uongo na watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaounga mkono serikali ya Congo. Kwa madai kuwa alipigwa risasi na pengine kuuawa wakati wa mapigano ya Goma.

Taarifa moja ya kupotosha ilihusisha madai kuwa kifo cha Nangaa ni kutokana na mashambulizi ya Jeshi la Afrika Kusini. Machapisho kadhaa yalidai kuwa Jeshi la Ulinzi la Afrika Kusini (SANDF), lilimuua Nangaa.

Taarifa nyingine zilidai kuwa Nangaa na Makenga walivamiwa na askari wa serikali ya Congo, na kujeruhiwa vibaya. Kulingana na akaunti hizi, wawili hao waliripotiwa kupelekwa Uganda au Rwanda kwa matibabu.

Ripoti hizi hatimaye zimethibitishwa kuwa za uwongo. Tarehe 29 Januari, Nangaa alinukuliwa vyombo vya habari vya Congo, akisema, lengo la waasi sio tu kuiteka Goma, bali ni "kuichukua Kinshasa na hatimaye kumwondoa madarakani Rais Tshisekedi."

Video ya uongo

Kesi nyingine ya habari potofu ilihusisha upotoshaji wa picha za video zinazomhusisha Bruno Lemarquis, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini DR Congo. Video hiyo ilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikiambatana na maelezo mafupi na sauti zinazodai kuwa Lemarquis alisema kuwa waasi wa M23 wameshambulia hospitali moja huko Goma na kuua akina mama wajawazito na watoto wachanga.

Lakini uchunguzi wa picha na muktadha wake ulifichua hitilafu kadhaa. Hakukuwa na ushahidi wa kuunga mkono madai kwamba Lemarquis alitoa taarifa kama hizo. Wala hakukuwa na ushahidi wa kushambuliwa hospitali wala hakukuwa na chombo cha habari cha kuaminika kilichoripoti, hata TV5Monde, ambayo ilielezwa kwa uongo kwamba ndio imepeperusha video hiyo.

Kuongezeka kwa taarifa za uongo juu ya mzozo wa Goma kunaonyesha ugumu wa kupata taarifa za kweli, huku wanaounga mkono serikali na wanaounga mkono waasi wakishiriki katika vita vya simulizi.

Habari potofu na habari za uongo imekuwa ni mbinu yenye nguvu ya kushawishi maoni ya umma, kuondoa uaminifu na kuvuruga juhudi za kutatua mzozo huo.

Wakati huo huo, serikali ya Kongo imefanya kuwa vigumu zaidi kwa vyanzo vya habari vya kuaminika kutoa ripoti ya kweli juu ya mzozo huo.

No comments