Muuguzi wa pili ashtakiwa kwa video ya kuwatishia wagonjwa Waisraeli

Muuguzi wa pili huko Sydney, Australia anayedaiwa kuonekana kwenye video inayotoa vitisho kwa wagonjwa wa Waisraeli amefunguliwa mashtaka na polisi.
Ahmad Rashad Nadir, 27, na Sarah Abu Lebdeh, 26, wote walisimamishwa kazi katika Hospitali ya Bankstown mwezi Februari baada ya video hiyo kuwekwa mtandaoni. Ilirekodiwa kwenye jukwaa la mtandaoni ambalo huwaunganisha watu kwa ajili ya gumzo.
Serikali inasema hakuna "ushahidi" kwamba wauguzi hao waliwadhuru wagonjwa.
Bw Nadir alishtakiwa Jumatano kwa kutumia mawasiliano kutoa vitisho na kukutwa na dawa iliyopigwa marufuku.
Sarah alishtakiwa wiki iliyopita kwa makosa matatu; kutoa vitisho vya vurugu kwa kikundi cha watu, kutumia mawasiliano kutishia kuua, na kutumia mawasiliano kufanya makosa.
Hakuna ambaye amepatikana na hatia ya mashtaka hayo, lakini Nadir aliomba msamaha mwezi uliopita kupitia wakili wake.
Katika video hiyo, ambayo inaonekana kurekodiwa ndani ya hospitali na kuchapishwa na mtengeneza maudhui raia wa Israel, Sarah na Nadir wanadaiwa kujisifu kwa kukataa kuwatibu wagonjwa Waisraeli, kuwaua, na kusema watakwenda motoni.
Video hiyo ilisambaa mtandaoni na kusababisha kelele za umma, huku Waziri Mkuu Anthony Albanese akiitaja kuwa "ya kuchukiza" na "mbaya."
Mapema mwezi huu Australia ilipitisha sheria kali dhidi ya uhalifu wa chuki kufuatia wimbi la mashambulizi ya chuki dhidi ya Wayahudi.
Pia kumekuwa na ongezeko la matukio ya chuki dhidi Uislamu. Kijana wa Australia alishtakiwa Jumatano baada ya kudaiwa kutishia kufanya shambulio kama lile la mauaji ya Christchurch kwenye msikiti wa Sydney.


No comments