Gallery

3/04/2025
efd

CHANZO CHA PICHA,REUTERS

Mpango mbadala wa ujenzi wa Gaza wa dola za kimareakani bilioni 53 (£41.4 bilioni) dhidi ya ule wa Rais Donald Trump wa Marekani wa "kuitwaa Gaza" na kuwaondoa Wapalestina zaidi ya milioni mbili, umeidhinishwa na viongozi wa nchi za Kiarabu katika mkutano wa dharura katika mji mkuu wa Misri Cairo.

"Mpango wa Misri sasa ni mpango wa nchi za Kiarabu," alitangaza katibu mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Ahmed Aboul Gheit mwishoni mwa mkutano huu wa saa moja.

Amesisitiza "msimamo wa nchi za Kiarabu ni kukataa uhamishaji wowote, iwe kwa hiari au kwa kulazimishwa."

Misri imetoa ramani ya mpango huo kwenye kurasa 91, ikijumuisha picha za vitongoji na majengo makubwa ya umma.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Rais wa Misri Abdul Fattah al-Sisi pia alitoa wito wa kuwepo kwa mpango sambamba wa suluhisho la mataifa mawili - taifa la Palestina pamoja na Israel.

Jambo hilo linaonekana na mataifa ya Kiarabu, na mengine mengi, kama suluhu pekee la kudumu la mzozo huu, lakini limekataliwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na washirika wake.

Mpango huu mpya unapendekeza kwamba Gaza itaendeshwa, kwa muda, na "kamati ya usimamizi wa Gaza chini ya mwavuli wa serikali ya Palestina.”

Swala la makundi yenye silaha kama Hamas, mpango huo unaeleza suala hili litatatuliwa ikiwa sababu za mzozo na Israel zitatatuliwa.

Baadhi ya mataifa ya Kiarabu yanataka kuvunjwa kabisa kwa Hamas; wengine wanaamini maamuzi hayo yanapaswa kuachiwa Wapalestina. Hamas inasemekana kukubali kuwa haitashiriki kuiendesha Gaza lakini imeweka wazi kuwa kuipokonya silaha ni mstari mwekundu.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, mara kwa mara amefutilia mbali ushiriki wowote wa Hamas, lakini pia hataki ushiriki wa Mamlaka ya Palestina.

Suala jingine nyeti la usalama katika mpango huo ni kutoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupeleka askari wa kulinda amani wa kimataifa.

Na mkutano mkubwa wa kimataifa utafanyika mwezi ujao ili kukusanya kiasi kikubwa cha fedha kinachohitajika kwa mradi huu wa kuijenga upya Gaza.

0 Comments:

Post a Comment