Subscribe Us

Breaking News

Watoto wenye umri wa mwaka mmoja ni miongoni mwa waliobakwa katika vita vya Sudan - UN


fc

CHANZO CHA PICHA,UNICEF

Maelezo ya picha,Hala (sio jina lake halisi) ni mmoja wa wasichana wengi waliobakwa tangu vita vianze

Watu wenye silaha wanabaka na kuwanyanyasa kingono watoto wenye umri hadi mwaka mmoja katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, linasema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, Unicef.

Unyanyasaji mkubwa wa kingono wa watu wengi umerekodiwa na kutumiwa kama silaha ya vita katika mzozo huo wa karibu miaka miwili.

Theluthi moja ya waathiriwa ni wavulana, ambao kwa kawaida wanakabiliwa na "changamoto” katika kuripoti uhalifu kama huo na kutafuta msaada wanaohitaji.

Unicef​​i nasema, ingawa kesi 221 za ubakaji dhidi ya watoto zimeripotiwa rasmi tangu kuanza kwa 2024, idadi halisi huenda ikawa kubwa zaidi.

Sudan ni nchi yenye uhafidhina katika jamii na hilo huzuia waathirika na familia zao kuzungumza juu ya ubakaji, kwa hofu ya kuadhibiwa na makundi yenye silaha.

Unicef inasema waathiriwa 16 wa unyanyasaji wa kingono walikuwa na umri wa chini ya miaka mitano, wakiwemo watoto wachanga wanne.

Unicef ​​haisemi ni nani anahusika, lakini uchunguzi mwingine wa Umoja wa Mataifa umewanyooshea kidole wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), inasema wapiganaji wa RSF walikuwa na mtindo wa kutumia unyanyasaji wa kijinsia kuwatisha raia na kukandamiza upinzani dhidi ya harakati zao.

RSF, ambayo inapigana vita dhidi ya washirika wake wa zamani, vikosi vya Wanajeshi wa Sudan, imekanusha kufanya makosa yoyote.

Kulingana na ushahidi uliowasilishwa na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu, wahanga katika ngome za RSF huko Darfur mara nyingi walilengwa kwa sababu walikuwa Waafrika weusi na si Waarabu, kwa lengo la kuwafukuza kutoka Sudan.

Kuna maelezo ya kutisha katika ripoti ya Unicef kama yale ya Omnia.

"Baada ya saa tisa usiku, mtu alifungua mlango, akiwa amebeba kiboko, akachagua msichana mmoja, na kumpeleka kwenye chumba kingine. Nilisikia msichana mdogo akilia na kupiga mayowe. Walikuwa wakimbaka," ameeleza Omnia (si jina lake halisi), mwanamke mtu mzima aliyenusurika baada ya kushikiliwa na wanaume wenye silaha katika chumba na wanawake wengine na wasichana.

"Kila mara walipombaka msichana huyu alikuwa akirudi akiwa ametapakaa damu. Ni mtoto mdogo tu. Wanawaachilia wasichana hawa alfajiri, na wanarudi wakiwa hawajitambui. Kila mmoja wao analia na kuongea ovyo. Katika siku 19 nilizokaa huko, nilifikia hatua ambayo nilitaka kukatisha maisha yangu."

Idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na vita imewafanya wanawake na watoto kuwa katika hatari zaidi ya kushambuliwa – Umoja wa Mataifa unasema, wasichana watatu kati ya wanne wa umri wa kwenda shule hawaendi shule.

No comments