Subscribe Us

Breaking News

Malcolm X: Jinsi mauaji yake yalivyotikisa Marekani miaka 60 iliyopita

 


fc

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,
  • Author,

Mwanaharakati wa kutetea haki za Wamarekani weusi nchini Marekani, Malcolm X, aliuawa tarehe 21 Februari 1965, akiwa na umri wa miaka 39.

Kukiwa na ulinzi mkali, maelfu ya watu waliokuwa kwenye mstari kuuaga mwili wake, walikuwa wakipekuliwa na polisi kama tahadhari dhidi ya milipuko.

Maono ya Malcolm X juu ya haki za watu weusi yaliwatia moyo watu wengi, huku yakiwatisha baadhi. Alikuwa maarufu kimataifa kwa maneno yake makali, lakini aliuawa wakati akibadilika na kuwa na mtazamo wa wastani.

Malcolm X aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa jukwaani kwenye ukumbi mmoja huko New York alipokuwa akijiandaa kutoa hotuba kwa Shirika lake la Afro-American Unity. Mke wake na watoto walikuwa kwenye hadhira.

Wanaume watatu waliopatikana na hatia ya mauaji yake wote walikuwa wanachama wa Nation of Islam, taasisi ya kisiasa na kidini, ambayo mwaka mmoja kabla, Malcolm X aliachana nayo huku kukiwa na uadui.

Mmoja wa watu hao alikamatwa wakati akijaribu kutoroka, na kukiri mauaji. Mwaka 2021, jaji wa jimbo la New York alikubali kuwa hukumu za wanaume wengine wawili hazikuwa sahihi. Wanaume hao wawili baadaye waliachiliwa huru.

Bado ni mtu mwenye utata miaka 60 baada ya kifo chake. Lakini kwa baadhi ya watu Malcolm X anasalia kuwa ishara ya hasira na upinzani mbele ya ukandamizaji.


Historia ya Malcolm

Alizaliwa kwa jina la Malcolm Little mwaka 1925 huko Omaha, Nebraska, alikuwa mtoto wa mhubiri wa Kibaptisti. Malcolm alipokuwa na umri wa miaka sita, baba yake aliuawa katika kile wengi wanachoamini ni shambulio la kimakusudi la ubaguzi wa rangi kutoka kwa wazungu wenye msimamo mkali. Ingawa hakuna anayejua kwa uhakika ukweli wa tukio hilo.

Mshtuko wa kuuawa kwa baba yake ulisababisha mama yake kupata mshtuko wa kiakili, na Malcolm na ndugu zake saba walisafirishwa na kupelekwa kwenye nyumba za kulelea watoto.

Alijiingiza katika maisha ya uhalifu, na mwaka 1946 alifungwa jela kwa kosa la kuiba. Akiwa gerezani, alianza kupenda kujifunza. Huko alikutana na mawazo ya Nation of Islam, taasisi ya kisiasa na kidini ambayo ilikuwa ikidai kuwa usawa kwa Wamarekani weusi ungeweza kupatikana tu kupitia watu weusi na weupe kuishi katika majimbo tofauti.

Alipoachiliwa kutoka gerezani mwaka 1952, alibadilisha jina lake rasmi na kuwa Malcolm X. Aliachana na jina la ukoo ambalo familia ililirithi kutoka vizazi vilivyotangulia, ambavyo vilifanywa watumwa.

Alizuru Marekani, akieneza ujumbe wa Nation of Islam, na kugundua kwamba alikuwa na uwezo na haiba ya kuwavutia watu kwa maneno yake. Kuzungumza hadharani ulikuwa ni ujuzi ambao alijifunza, baada ya kuingia gerezani baada ya kuacha shule ya kati.

Hakuogopa kutumia mbinu za maneno ya kushitua kufikisha ujumbe wake, akiwashutumu wazungu kuwa ni "shetani mweupe" kwa ukandamizaji wa kihistoria wa watu weusi. Rais wa Marekani John F Kennedy alipouawa Novemba 1963, alisema, "amevuna alichopanda."

Wakati Malcolm X akivutia wafuasi wengi, pia alitengeneza maadui wengi. Machi 1964 alitangaza anaachana na Nation of Islam, baada ya kukatishwa tamaa na uongozi wake.

Mwezi huohuo, alihudhuria mjadala huko Washington DC kuhusu Mswada wa Haki za Kiraia, na hatimaye alikutana na Martin Luther King, Jr, kiongozi wa haki za kiraia ambaye alikuwa ni muumini wa maandamano yasiyo na vurugu – jambo ambalo lilionekana kuwa tofauti kabisa na falsafa ya Malcolm X ya makabiliano ya ana kwa ana.

Ili kuimarisha imani yake ya Kiislamu, alikwenda kuhiji Makkah. Aliandika kuhusu jinsi alivyoshuhudia, "mahujaji wa rangi zote kutoka sehemu zote za dunia hii wakionyesha roho ya umoja na udugu. Jambo ambalo sijawahi kuona."

Pia alizuru nchi kadhaa barani Afrika, na kufanya uamuzi wa kuunda kikundi kipya kisicho cha kidini, ili kujaribu kuwaunganisha Waamerika wenye asili ya Afrika na asili yao.

Aliporejea Marekani, aliachana na mafundisho ya Nation of Islam. Ndipo wakati huo, mke wa Malcolm X, Betty Shabazz, alipoanza kupokea vitisho vya kuuawa kupitia simu, na nyumba yao ilishambuliwa kwa bomu.

Licha ya vitisho kutoka pande nyingi, aliendelea kujitokeza hadharani. Juni 1964, alizindua rasmi Shirika lake la Afro-American Unity, akiwaambia wasikilizaji waliokusanyika: "Tunataka uhuru kwa njia yoyote ile. Tunataka haki kwa njia yoyote ile. Tunataka usawa kwa njia yoyote ile."

Ukumbi ulikuwa ni Audubon Ballroom, katika kitongoji cha Washington Heights katika jimbo la New York. Na miezi minane baadaye aliuawa katika jukwaa hilo hilo.

Kubadili msimamo

Malcolm X alikuwa mgeni wa mara kwa mara katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, kulingana na Daniel Watts, mhariri wa jarida la wazalendo weusi la The Liberator.

Anasema "nadhani kwa mara ya kwanza katika historia ya mapambano hapa nchini, tulikuwa na mtu aliyetupa matumaini."

Mshairi Maya Angelou alikuwa rafiki wa Malcolm X, na walikuwa wote wakati wa safari yake ya Afrika alipotembelea Ghana, ambako Angelou alikuwa akiishi wakati huo. Akizungumza mwaka 1992, aliiambia BBC:

"Alikuja Ghana na kusema, "nimekutana na watu wenye macho ya buluu ambao ninaweza kuwaita ndugu, hivyo kauli yangu ya awali kwamba wazungu wote ni mashetani, ilikuwa ni potofu.' Inahitaji ujasiri wa ajabu kuweza kusema, 'mnakumbuka nilichokisema jana, nimegundua kuwa si sahihi.' Na hilo ndilo aliloweza kufanya.

Malcolm X alifariki akiwa katika safari ya kubadili misimamo yake na kuwa na misimamo ya wastani. Sijui alikuwa na wafuasi wangapi, lakini alikuwa na watu wengi wanaomtakia mema.

No comments